Simu nyingi za kisasa huja na programu ya kucheza muziki. Programu hii inatosha kwa mambo ya msingi lakini vipi kama unahitaji muonekano tofauti au mambo mengine matamu zaidi kama kucheza muziki punde unapochomeka hedifoni na kupata picha za wanamuziki sanjari na nyimbo zako?
Tunachambua app 5 bomba za muziki kwa ajili ya simu yako ya kijanja.
Rocket Player
Ni jambo rahisi sana kuanguka kimapenzi na muonekano wa Rocket Player. Ukiifungua, nyimbo na picha hupangiliwa kwa umaridadi sana. Utapenda jinsi ilivyo rahisi kutafuta nyimbo uipendayo kwa kusogeza skrini juu-chini, kushoto na kulia. Cha kufurahisha zaidi ni kwamba ukichomeka tu hedifoni, Rocket Player inaanza kucheza muziki. Hii inasaidia sana. Chukua picha kama uko kwenye jua kali na hauoni skrini au labda hautaki tu kufungua skrini. Appu hii ina skrini yake inayotokea kabla ya kuifungua simu ili kukupa urahisi wa kubadili nyimbo haraka. Ukifuatilia mipangilio yake kwa umakini na kupambana na kiingereza kidogo, utaweza kubadili muonekano wa Rocket player kwa kuipa rangi unayotaka, kulazimisha nyimbo zianze kucheza kwa sauti ya kiwango unachotaka unapochomeka hedifoni na kulipia huduma zaidi kama ya kutumia hifadhi-pepe (cloud) na kushusha picha za wanamuziki. Rocket Player inaweza pia kufungua na kucheza video. Kiukweli, hii app imekamilika.
Shuttle Player
Shuttle Player ni appu inayofanana sana na Google Play Music Player inayopatikana kwenye simu nyingi za Androidi. Sifa kubwa ya appu hii ni uwezo wa kushusha picha za wanamuziki bure kwenye kitumi chako ili zionekane pale unapocheza muziki. Kama Rocket Player, Shuttle inaweza kucheza muziki unapochomeka hedifoni ila huduma hii inawezekana pale unapoingia kwenye mipangilio na kuiwezesha. Jambo lingine la kipekee kwa appu hii ni uwezo wa kutuma nyimbo kwa urahisi kwenda kwa mtu mwingine. Zaidi ya huduma hizo, Shuttle ni rahisi kuielewa na kutumia. Ina mpangilio wa kuridhisha unaorahisisha kutafuta nymbo kirahisi na inatumia rasilimali za simu kidogo kulinganisha na appu pinzani.
aePlayer
aePlayer inakuweka karibu zaidi na nyimbo unazozipenda. Kinachofanyika ni wewe kuiambia kuwa unapenda nyimbo flani kwa kubonyeza kialama cha moyo juu ya nyimbo zinazocheza na yenyewe itakupa orodha ya nyimbo hizo punde unapoifungua app hiyo. Pili, inakupa orodha ya nyimbo ulizoziweka muda si mrefu uliopita. Zaidi ya hapo, aePlayer ina uwezo wa kushusha picha za wasanii na kuziambatanisha na nyimbo zako pale zinapocheza.
DoubleTwist
Kama unapenda muonekano wa kuvutia, Double Twist ni kwa ajili yako. vigumu kupata appu nyingine iliyo na muonekano maridadi na usio mzito kama wa appu hii. Kwa DoubleTwist unaweza kusikiliza vipindi na redio za ughaibuni na kubadili muziki punde unpowasha skrini bila kuifungua (Lockscreen control). Jambo lingine linaoiweka DoubleTwist mbele ni urahisi wa kuwashirikisha marafiki wa facebook na Twitter kuhusu nini unakisikiliza kiurahisi. App hii inajiunga moja-kwa-moja na facebook ukiiruhusu. DoubleTwist inapambanisha na Rocket Player kwa uzuri ila Rocket player inatisha zaidi kwa uwezo wa kuweza kucheza muziki ukichomeka hedifoni.
musiXmatch Player
Musixmatch ni baba lao ikija kwenye appu za muziki kwenye Androidi. Appu hii inakuonesha maneno ya nyimbo(lyrics) za nyimbo, unaweza kujisikiliza wakati unaimba nyimbo na untaweza kugundua nyimbo ambazo huzifahamu kwa kuisikilizisha simu nyimbo hiyo. Pamoja na hayo, unaweza kuipangilia simu kucheza au kusimamisha muziki punde unapochomeka au kutoa hedifoni na kubadili nyimbo bila kufungua simu. Thadhari pekee ni kwamba musixMatch inaweza ikawa nzito kwenye simu yako na kwa sababu hiyo, unaweza usiifurahie kama simu yako ni ya uwezo mdogo au kawaida.
Ziada
Rocket, Shuttle, aePlayer, Doubletwst na musixMatch ni baadhi tu ya chaguo letu la appu 5 bomba kwa muziki kwenye simu na tableti za Androidi. Nyingine ya kuangalia ni n7 yenye muonekano ambao ni tofauti sana,mediaMonkey na VLC ambazo bado zinafanyiwa matengenezo na zitabadilika kila mara na nyingine nyingi ambazo kila moja ina sifa zake. Endelea kufurahia chaguo la appu za Androidi kutoka Teknokona.
Picha Na:
icaruswept.com,play.google.com,m.new-day-apps.store.aptoide.com, androidapphut.com, www.elandroidelibre.com
No Comment! Be the first one.