Tanzania ni moja ya mataifa ambayo twitter inakua kwa kasi kubwa sana duniani. Twitter ni mtandao wa jamii amabao unatumika kushirikisha watu hasa kwa habari za kushtua (‘breaking news’) na matukio ya laivu. Huu mtandao ulianzishwa mwaka 2006 na Jack Dorsey, Noah Glass, Evan Williams na Biz Ston na tangu kipindi hicho twitter imekuwa mtandao mkubwa unaotumiwa na watu wengi maarufu na makampuni mengi duniani.
Ingawa twitter inatumika na watu wengi duniani, moja ya vitu inavyoifanya iwe nyuma zaidi ya mitandao mingine ya kijamii kama facebook na instagram ni kwamba si mtandao rahisi sana kuutumia na kuuelewa. Kuna mambo machache muhimu mtu inabidi ujue kabla ya kuanza kutumia twitter na hata baada ya kuitumia, jinsi ya kuitumia vizuri. Tuangalie sasa jinsi gani unaweza kuitumia twitter au kuongeza utamu wa kutumia:
1. Nijiunge au niiache inipite: Kwa nini twitter?
Watu hutumia twitter kupashana habari na kuieneza kwa haraka na cha muhimu zaidi, mtandao huu inatumika kuzungumzia jambo linaloendela laivu na siyo jambo lililopita, kwa hiyo kama unataka kujiunga na twitter, jitaharishe kuwa chonjo mtandaoni na kuwa katika matukio tofauti unayoyapenda. Pia, twitter inatumika katika maongezi ya papo kwa hapo na makampuni mbalinbali kama stesheni za radio na tv kwa ajili ya kukusanya maoni na mitazamo ya wasikilizaji au wateja wao. Unaweza kuitazama kama mbadala wa sms ambao ni wa kasi zaidi na nafuu zaidi kwa mtumiaji. Kuweka mambo sawa, ni sahihi kusema kama wewe siyo mtu wa kufuatilia matukio fulani fulani ya hapo kwa hapo, au si mtu wa kujichanganya na wengine katika maongezi basi twitter haitakufaa sana.
2. Elewa kutumia lugha ya twitter ili ‘tweet’ zako zionekane zaidi.
Twitter hutumia mfumo wa ‘hashtagi’ ambao unatumika kukusanya ‘tweet’ zinazozungumzia tukio au mjadala mmoja. Hizo hashtagi zinaweza kutolewa na utawala unaoshughulikia tukio zima au unaweza kuibuka kwa mmojawapo wa washiriki na ukadakwa na watu. Ukiachana mbali na hashtagi, kuna matumizi ya @. Hii inatumika kumtaja mtu na kumshirikisha kwenye mazungumzo yako tweet-ani. Unapomtaja mtu, anapata kuona maoni yako na kuweza kukujibu kwa kutmia jina lako la twitter pia. Mbali na kutumika katika mazungumzo, hashtagi na @ zinaweza kutumika pia kutafuta akaunti na mijadala ya watu kupitia ‘search-bar’.
3. Fuatilia mambo yanayokuvutia au kukupendeza.
Hii inaweza ikawa kufuatilia watu, makampuni au mashirika yanayokupendeza/ungependa kujua masuala yanayojitokeza kwao. Moja ya mambo ambayo watu hufanya na hawayafurahishi kwenye twitter ni kuwafuatilia watu wengi mpaka home-feeds zao inakuwa na vitu ambavyo havimsaidii na havimuendelezi zaidi ya kumchukiza. Jambo la makini kufanya ni kufuatilia watu wachache ambao vitu wanavyofanya maishani vinakupa furaha na hamasa ya kujua na kuwafuatilia. Ila kama inakubidi ufuate akaunti nyingi kwa kuwa zote ni muhimu basi pointi inayofuatia ni muhimu uitekeleze – Lists.
4. Tumia Lists kupangilia mijadala, watu au makampuni unayopenda kufuatilia
Moja ya vitu ambavyo vinasaidia sana kwenye utumiaji wa twitter ni lists. Hii inasaidia sana wale watu ambao hawana muda wa kushiriki kwenye matukio ya hapo kwa hapo muda wote lakini baadae wanataka kujua yaliyojiri kutoka kwa watu au makampuni wanayofuatilia. Kwa mfano, ninafuatilia habari za tanzania. Nitatengeneza List ya ‘Habari za Nyumbani’ na kuweka watu kadhaa na magazeti kadhaa ya tanzania amabo nafuatilia. Nikiingia twitter mwisho wa siku, naachana na home-feed yangu na kufungua list yangu ya habari za Tanzania na kupata kwa haraka, vichwa vya habari vyote siku ya leo. Pia pale unapokuwa unapokuwa unafuatilia akaunti nyingi uwepo wa Lists (Orodha) ya watu wenye umuhimu zaidi kwako itakusaidia kuwafuatilia kwa uraisi zaidi.
5. Tengeneza Profile yako vizuri.
Jambo litakalokuweka kwenye chati kwenye mtandao wote ni maelezo yako binafsi, yani ‘profile’ yako. Hilo ni kama sura yako, kama itapendeza basi utawaalika watu wengi zaidi, na kama sivyo, basi jitahidi tena. Badilisha-badilisha kuona nini kitawavutia watu wakufuatilie. Ila zaidi ya yote onyesha uhalisia.
6. Unga twitter na facebook.
Kuunga twitter na facebook kutaongeza chachu ya kutumia twitter. Itakupunguzia adha ya kutoka twitter na kuingia facebook na tena kurudi twitter, utaua ndege wawili kwa jiwe mojai. Unataka kujua ujanja huu – Tuliandika hapa.
7.Tumia huduma nyingine na app zingine za Twitter.
Utamu wa kutumia twitter ni kwamba haulazimishwi kutumia programu iliyotolewa rasmi na kampuni. Unaweza kujaribu programu nyingine kadhaa kwa kitumi chako na kujionea utafauti wa ku-tweet nazo na kuona tweet za watu wengine pamoja na mambo mengine ya twitter. Kwa Android, programu zinazoongoza ni TweetCaster, Plume na Twidere. Kwa i-phone na i-pad, unaweza kujaribu tweetdeck na twitterrific na kwenye Windows, Tweetium na tweetdeck.
Kwa makala hii ndefu kidogo, tunatumaini utaufurahia twitter zaidi au tumekusaidia kuungana na mamia ya Watanzania na watumiaji wa kiswahili duniani amabo wanatumia mtandao huu. Je, unataka kujua nani magwiji wa twitter hapa nyumbani na duniani? Endelea kusoma.
Mwanamziki mmarekani, Katy Perry ndie anayeongoza kwa kuwa na wafuatiliaji wengi zaidi duniani kwenye mtandao wa Twitter(millioni 56), akifuatiwa kwa karibu na mwanamziki mwingine, bwana mdogo Justin Bieber. Hapa kwetu Tanzania, akaunti inayoongoza ni ile ya raisi wa nchi (wafuatiliaji 178,352), akiwa pia ni miongoni mwa wanasiasa wanaofuatiliwa zaidi Afrika. Millard Ayo anaongoza kwa wanahabari na kwa upande wa wanamuziki, basi mwanamuziki kinara ni A.Y (Ambwene Yesaya ).
No Comment! Be the first one.