Baada ya kufanikiwa kuliteka na kulimiliki soko kwa takribani muongo mmoja ghafla taratibu mauzo yanapungua na kuanguka kabisa sokoni. Inashangaza na kushtua kidogo kuona kampuni kubwa ya simu ya Nokia iliyojizolea umaarufu mkubwa sana duniani ikitapatapa walau kupata asilimia ndogo tu yaani angalau asilimia moja ya sehemu ya soko la simu janja duniani!.
Tukirudi nyuma kidogo Miaka takribani kumi iliyopita yaani miaka ya 2000 kurudi nyuma soko zima la simu lilishikiliwa na Nokia hadi kusababisha kuwa kampuni ya kwanza kuvunja rekodi ya kuuza simu nyingi duniani na kumpiku Motorola ambaye alikua mpinzani wake sokoni. Je, nini kilitokea mpaka Nokia ikaanguka? Songa na mimi kuweza kufahamu kuhusu anguko la Nokia.
Historia fupi ya Nokia
Mnamo mwaka 1992, Novemba 12 Nokia waliingiza toleo lao la kwanza la simu ya mfumo wa ulimwengu wa rununu (GSM) sokoni waliyoipa jina la Nokia 1011 ambayo ilikua na uwezo wakupiga/kupokea simu pamoja na ujumbe tu ambayo iliundwa kwa mfumo wa kubonyeza vitufe ili kuitumia (goroka) simu hii ilifanikiwa kuteka soko vibaya mno duniani iliongoza kufanya vizuri sana kwa mauzo kwa miaka hio.

Nokia waliendelea kuachia matoleo mengine kama Nokia 1100 na Nokia 1110 ambayo yaliuza sana na yalifanya vizuri sokoni kuzidi hata lile toleo la kwanza pia walitoa simu janja kama Nokia Lumia, Nokia Asha, Nokia X, Nokia 7 plus mpaka Nokia 9 Pure View.

Mambo yaliyosababisha nokia kuanguka
Mabadiliko katika Usimamizi wa Juu
Mnamo 2006, Mkurugenzi mtendaji wa Nokia, Bw. Jorma Ollila alibadilishwa na nafasi yake alipewa Olli-Pekka Kallasvuo kama Mkurugenzi Mtendaji mpya. Usimamizi huu mpya chini ya Olli-Pekka Kallasvuo ulisikiliza sana mahitaji ya wateja wake ambao walihitaji zaidi simu za jadi hivyo walitia nguvu nyingi kutengeneza simu za rununu za Nokia, na matoleo yote yalizingatia zaidi simu za jadi badala ya kujaribu teknolojia mpya.
Kushindwa kubadilika kwa wakati
Licha ya kujua kwamba kulikuwa na mahitaji zaidi ya programu kuliko vifaa sokoni, Nokia walilifumbia macho hili. Na ndipo Mwaka 2007 kampuni ya apple wanakamata fursa nakujikita zaidi kwenye utengenezaji wa simu janja aina ya iPhone (iOS) ambazo zilikua na uwezo wa 2G pia soko lake lilikuwa dogo pia halikua la uhakika kutokana na wateja walikua bado hawajalielewa, hivo nokia hawakujisumbua sababu tayari soko lake lilikuwepo la uhakika na simu zake zilikua na uwezo wa 3G hivyo walipuuzia teknolojia mpya.
Mwaka 2008, kampuni ya Google nao walianzisha mfumo endeshi (Android) Lakini bado Nokia walipuuzia nakuendelea kutumia mfumo endeshi (Symbian OS) ambao ulikua wa kizamani. Hii ilifanya kampuni hizo za Google na Apple kukua taratibu na kuzoeleka sokoni mpaka kuteka soko. Wakati Nokia wanagundua makosa yao, walikuwa wamechelewa kidogo kwa sababu watu walihamia kwenye simu za Android na Apple.
Kujiamini kupita kiasi na dharau
Usimamizi wa juu wa Nokia ulidhani kuwa hakuna kitu kinachoweza kwenda vibaya hivyo hawakua na haraka na mpango wa teknolojia mpya mpaka watakapo amua kufanya hivyo. Na ndipo kampuni mpya zilikuja na maoni kuhusu teknolojia mpya ila Nokia walizipotezea kutokana na uchanga wao. Walishindwa kuwekeza kwa wakati huo zaidi kwenye teknolojia mpya, hawakufikiria mtu yeyote angeweza kushindana nao. Walijiamini kupita kiasi na kuyadharau makampuni mapya na hapo ndipo walipokosea.
Ushirikiano na Microsoft
Mnamo 2011, Nokia wanaingia ubia na Microsoft kutengeneza simu janja za Windows, na kuachana na mfumo endeshi wa zamani kama Symbian na MeeGo. Mnamo mwaka wa 2012, simu za Windows zinashindwa ushindani sokoni sababu kuu ilikuwa uwepo wa idadi ndogo za programu kwenye duka la windows ukiilinganisha na zinazopatikana Playstore na AppStore.
Kununuliwa na Microsoft
Mnamo mwaka 2014, Nokia ilikuwa karibu kufilisika lakini Microsoft iliinunua Nokia kwa $7.2 bilioni. Hii ilitumika kama ishara na ushahidi tosha wa anguko la mwisho la kampuni hii kubwa maarufu na yenye nguvu duniani ya Nokia.
Licha ya kuanguka kwake lakini bado Nokia wameendeleea kutoa matoleo mengine ya aina tofauti tofauti ya simu kwa ajili ya wateja wake wadamu ingawa ushindani sokoni hajafanikiwa kabisa kuuweza mpaka sasa kutokana na makampuni mengi mapya kuja juu kwa kasi kali sana na teknolojia ya viwango vya hali ya juu.
Je, unavyoona Nokia ataweza kushindana huu mchuano mkali uliopo sokoni wa simu janja wa baadhi ya simu kama huawei, Apple, xiaomi, OnePlus, Redmi na Samsung akafanikiwa au la?!. Dondosha maoni yako hapa.
Chanzo: Programmer
No Comment! Be the first one.