Windows 10 haitaingilia kazi mara kwa mara kukutaarifu kupakia ‘Anti-virus’ kwenye mashine yako kama vile Windows 7 ilivyokuwa ikifanya. Hii ni kwa sababu kuanzia Windows 8, Microsoft walifanya uamuzi wa msingi wa kuweka Anti-virus moja-kwa-moja kwenye mfumo wao. Antivirus hii inaitwa Windows Defender na ni Antivirus ambayo Microsoft wenyewe wanaitoa bure pamoja na WIndows mpya. Kwa maana hiyo swali la msingi la makala hii linafaa kubadilika na kuwa – ‘Je Windows Defender ni antivurus ni bora zaidi kwa usalama wa kompyuta yako au la?’
Windows Defender
WIndows Defender inatokana na Microsoft Security Essentials (MSE) na ni, kwa maneno mengine, toleo la kisasa zaidi la MSE, ambayo ilikuwa ni antivirus ya bure kabisa kwa ajili ya Windows 7. Kwa sasa, antivirus ya Windows Defender inakuja pamoja na Windows na ni ngome ya kwanza kwa kompyuta yako.
Je, Windows Defender Inatosha?
Unapoanza kutumia Windows 10, Windows Defender nayo huanza kufanya kazi moja-kwa-moja na ku-scan kila programu unayofungua na kwa mpangilio wa kawaida, inaji-sasisha yenyewe unapojiunga na mtandao. Kwa kawaida Windows Defender haionekani wazi ikifanya kazi ila unaweza kupata ripoti ya kina zaidi ya usalama wa kompyuta yako ukitaka kwa kuifungua Windows Defender, kwa kuitafuta kwenye orodha ya programu zako kwenye ‘Start Menu’.
Kiujumla, watalamu wengi mtandaoni husema kwamba anti-virus za Microsoft zipo nyuma kidogo ya nyingine zenye ushindani, hata-hivyo, Windows Defender ina faida lukuki.
Defender inakuja moja-kwa-moja na Windows na inafanya kazi kimya-kimya (haina usumbufu wa matangazo mara kwa mara) na haitumii rasilimali nyingi. Pia, haitatumia data zako za kwenye kivinjari, zinazotumika kujaribu kutengeneza faida kama vile inavyofanywa na makampuni mengine yanayotoa antivirus bure.
Windows Defender siyo mbaya sana kwa usalama kompyuta yako iwapo ukizingatia mambo machache kama kusasisha kompyuta na kivinjari chako na pia kuepuka kutumia programu hatarishi kama kiwezeshaji cha java (‘java plugin’).
Kwenye matokeo ya AV-Test, Windows Defender ilipata 0.5 / 6 kwa usalama, huku ikikamata 95% ya virusi na programu hatarishi (“widespread and prevalent malware”) mnamo June mwaka huu, pamoja na 85% ya virusi vya siku hadi siku. Ukilinganisha, BitDefender iliweza kakamata asilimia 100 na 100 ya sampo, huku Kaspersky ikikamata asilimia 100 na 99. Kwa mantiki hiyo, pamoja na utofauti kati ya matokeo hayo, Windows Defender bado ina usalama wa kuaminika. Microsoft wenyewe wamekuwa wakisikika wakiweka wazi kwamba dhumuni lao ni kushughulika na programu hatarishi na virusi vinavyoathiri kompyuta nyingi na ni tofauti na watengenezaji wa antivirus ambao wanashindana na virusi vya kila siku na hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya kushinda majaribio yoyote.
WIndows 10 pia ina usalama wa aina tofauti pia, ambao ulianza kutumika katika Windows 8 kama SmartScreen filter ambayo inakuzuia kushusha na kupakia programu hatarishi, hata kama ukitumia antivirus tofauti na ya Microsoft. Chrome na Firefox nazo huwa na ‘Google’s Safe Browsing’, ambayo inakuzuia kushusha programu hatarishi.
Kiujumla, Windows Defender inaweza kuwa sawa tu kwa watumiaji wa kawaida. Hili ni pamoja na kuzingatia hatua chache za kujilinda. Ilani lakini, kama wewe ni mtumiaji wa programu ambazo siyo kutoka vyanzo vya kuaminika (kama torrent) na unafanya mambo mengine hatarishi kwa kompyuta yako, unashauriwa kutafuta antivirus nyingine yenye uwezo zaidi.
Tumia MalwareBytes Anti-Exploit Pia
Kama ziada unashauriwa sana kutumia programu maalumu ya kuzuia mashambulizi yanayoelekezwa kwenye kivinjari na visaidizi vyake. Hivi hulengwa sana na wadukuzi wa mtandao. MalwareBytes Anti-Exploit ni mfano wa programu kama hii, na ni ya bure ambayo unashauriwa kutumia. MalwareBytes kazi sawa na programu ya Microsooft iitwayo EMET security tool, lakini ina utofauti wa kuwa rahisi zaidi kutumia na ina vipengele vingi zaidi vya usalama. Hizi zana zinasaidia kuzuia mbinu nyingi zinazojulikana za ki-udukuzi. MalwareBytes Anti-Exploit inaweza kuzuia hata yale matatizo ya kiusalama ya Adobe Flash yanayosikika mara kwa mara.
Windows Defender ikitumika sanjari na MalwareBytes Anti-Exploit ni suluhisho tosha na la nafuu unaloshauriwa kutumia kufanya kompyuta ya mtumiaji wa kawaida wa Windows 10 kuwa salama. Watu wanaotumia Windows 10 kwenye kompyuta za kiofisi zaidi wanaweza kuweka Windows Defender ikishirikiana na Microsoft EMET, ila Windows defender na MalwareBytes Anti-Exploit ni njema zaidi kwa kompyuta za kawaida. MalwareBytes Anti-Exploit pia inaweza kutumika na anti-virus nyingine yoyote na itakamata programu hatarishi na programu nyingine ambayzo hazihitajiki (zinazolazimisha kujiweka zenyewe) na zile ambazo anti-virus huwa hazikamati.
Lakini Antivirus Ipi Ni Bora zaidi?
Sawa, labda hauja-ielewa Windows Defender sana na unataka kitu kingine chenye jina kubwa.
Kwenye swali hilo kuna majibu mawili: Kama unatafuta anti-virus ya kulipia, Kaspersky na BitDefender kwa kawaida huwekwa kati ya anti-virus 3 nzuri zaidikatika majaribio mengi ya antivirus.
Kama unatufuta antivirus ya bure, Windows Defender bado ni jibu tosha. Bado kama moyo wako unaenda kwenye anti-virus nyingine unazojua za bure, hakikisha antivirus hizo haziweki kitu kwenye kivinjari chako au kukuwekea programu nyingine amabazo pengine hupendi au hutumii. Hivi vyote huwekwa ili kulipia kile wanachosema kwamba ni bure (hakuna kitu cha bure aisee, ni ujanja tu). Wanalipaje? Wanatumia data zinazopatikana kwa wewe kutumia programu hizo zinazojilazimisha kwenye kivinjari au kompyuta yako – kwa maneno mengine, wanauza data kuhusu unatumiaje programu hizo.
Windows Defender itaacha kufanya kazi unapoweka anti-virus nyingine kutoka kampuni tofauti na Microsoft na kujirudisha tena pale unapotoa anti-virus tofauti. Windows Defender imetengenezwa kutokubughudhi.
Neno la Mwisho
Kwa antivirus yoyote utakayoweka, tegemea kwamba hautakuwa salama asilimia 100. Kama umezoea kushusha na kupakia programu hatarishi, ipo siku utaingia matatani. Kuweka antivirus bora ni jambo la kukupa amani kwamba uko salama ila kama haufuati taratibu za matumizi salama ya kompyuta – ni kazi bure. Na katika dunia ambayo, kirusi cha kuogopa zaidi ni kile kisichojulikana kabisa kile kinacholenga kivinjari, MalwareBytes Anti-Exploit inaweza kuwa kimbilio bora zaidi kwa usalama wa kompyuta ya Windows 10 kuliko kukimbilia antivirus nyingine zaidi ya Windows Defender.
Chanzo: HowToGeek
No Comment! Be the first one.