Unatafuta njia rahisi ya kuhakikisha simu yako inakaa na chaji muda mrefu zaidi na inakuwa nyepesi kiutendaji? Basi ondoa kwa lugha nyingine ‘uninstall’ app ya Facebook kutoka kwenye simu yako.
Ni kweli ni mtandao wa kijamii unaoongoza sana kwa watumiaji na pia ukiwa na pesa lukuki lakini inaonekana bado watengenezaji wake wa app yao kwa toleo la simu za Android bado hawajaweza kujua jinsi ya kufanya app hiyo ifanye kaze zake kwa ufanisi mzuri zaidi.
‘Ufanisi’ tunamaanisha kutumia kiwango kidogo cha chaji na nguvu kazi ya simu.
Waandishi wa mitandao miwili, The Guardian na Android central – kwa wakati tofauti wamefanya utafiti huu mdogo ambao pia sisi pia tumeujaribu na unaonekana kwa kiasi kikubwa ni kweli… Unapokuwa na app ya Facebook upunguaji wa chaji unaongezeka, na pia kama simu yako ina uwezo mdogo wa kiutendaji basi tegemea uzito flani katika utumiaji wa simu hiyo.
Facebook App ulaji wa Chaji na Kufanya simu kuwa nzito
Kwa kipindi kirefu watu wengi wameshalalamika sana kwa nini toleo la app ya Facebook kwa simu na tableti za Android linatumia nguvu nyingi kufanya kazi ukilinganisha na toleo la app hiyo kwa vifaa vya iOS (iPad na iPhone). Na inaonekana kwa kiasi kikubwa app hiyo inatumia chaji nyingi pale ambapo ata inapokuwa haitumiki na mtumiaji – kitu kinachofahamika kwa jina la ‘Background process‘. Ni sababu hizo mbili ndio zinazochangia kwa kiasi kikubwa utumiaji wa chaji kwa app hiyo.
Na ubaya ni kwamba ata ukienda kwenye eneo la ‘Power Management’, sehemu kwenye mipangilio (settings) ya Android unapopata picha halisi ya utumiaji wa chaji wa apps mbalimbali – utaona ya kwamba utumiaji wa chaji wa app hiyo ya Facebook si mkubwa sana.…ila wachunguzi wamegundua kuna mambo mengi ambayo app hiyo inayafanya kutumia mgongo wa programu endeshaji ‘ Android System’, na hivyo utumiaji wa chaji huo uwa unaripotiwa kama ni wa programu endeshaji (system) badala ya app ya Facebook.
Inaonekana pia pale apps za Facebook na Facebook Messenger zikitolewa kwenye simu apps nyingine zilizobakia zinafunguka kwa uharaka wa takribani asilimia 15 zaidi ukilinganisha na hali yake kabla. Hii ikionesha ya kwamba apps za Facebook na Facebook Messenger zinafanya simu kuwa nzito.
Tatizo la apps za Facebook – ile ya kawaida na Messenger kulifanya hadi mmoja wa mabosi wa mtandao huo kulazimisha watengenezaji wao wa app hiyo kutumia simu za Android tuu kazini na kuachana na za iPhone ili tuu waweze kuona na kufahamu kwa undani matatizo wanayoyapata watumiaji wa app hizo kwenye simu za Android.
Kama tayari simu yako ina matatizo sana ya kukaa na chaji basi unaweza kutumia app nyingine mbadala zinazokupatia huduma zote muhimu za Facebook, mfano Metal. App ya Metal inakupatia uwezo wote muhimu wa huduma ya mtandao wa Facebook ila ikitumia kiwango kidogo zaidi cha chaji ukilinganisha na app rasmi ya Facebook.
Je wewe ni mtumiaji wa app ya Facebook kwenye simu yako? Tuambie kama ushawahi kuiondoa na kuona tofauti nzuri ya utumiaji wa chaji kwenye simu yako.
Na je upo tayari kuondoa app hiyo ili tu uweze kuwa na chaji muda mrefu zaidi?
Vyanzo: The Guardian, AndroidCentral na mitandao mbalimbali
2 Comments