Mwezi uliopita mtandao WhatsApp uliacha ku-support app yao kwa simu za Blackberry, Facebook nao wafanya maamuzi hayo nao pia wameondoa ‘support’ yote kwa simu za BlackBerry zinazotumia programu endeshaji yao.
Kusitishwa kwa support kuna maana kwamba watumiaji wote wa Facebook ambao wanatumia vifaa vya Blackberry ambavyo vinatumia OS ya Blackberry hawataweza kusawazisha mawasiliano (ama namba za simu) na pia hawataweza kusambaza picha moja kwa moja kwa kitufe cha ku-share.
Lakini zaidi ni kwamba Facebook hawatatengeneza matoleo mapya kwa ajiri ya watumiaji hawa tena, hii ni sawa na kusema kwamba watumiaji hawa watatakiwa kutumia web kupata huduma hizi.
Katika post ambayo BB wameiweka katika blogu yao wanasema kwamba wamesikitishwa sana na maamuzi haya hasa kwa sababu wanajua kwamba wana watumiaji wengi ambao wanazipenda app hizi, na wamepigania sana kuwafanya WhatsApp na Facebook kurudisha support lakini maamuzi ya mitandao hii imebaki palepale.
Hata hivyo Blackberry mwishoni mwa mwezi huu wataleta app mbadala sio tu kwa app ya Facebook bali pia hata WhatsApp ambayo app hii itakuwa inawa-direct watumiaji katika matoleo ya mtandao huo ya web. Hivyo watumiaji wa simu zenye OS ya Blackberry wasitupe simu zao mapema.
Simu za Blackberry zilipata umaarufu wakati zipo katika chati, ujio wa Android na iPhone umekuwa ni kama ujio wa ruba katika bwawa ambalo Blackberry walikuwa wanajivunia.
Kitu kilichoiweka Blackberry mpaka leo ni watumiaji ambao ni waaminifu kwa OS na pamoja na kushuka kwa mauzo wenyewe wameendelea kutumia simu hizi tu, lakini wataalamu wa mambo wanasema kwamba pengine kuondoka kwa Facebook pamoja na whatsApp ikawa ndio mwisho wa kijiwe cha Blackberry.
Hivi karibuni BlackBerry walishaonesha nia ya kutumia programu endeshaji ya Android katika simu zijazo ili kuendelea kuwa na maana katika soko la simu. Bado haijajulikana rasmi kama simu yao ya Priv inayotumia Android imefanikiwa kimasoko kiasi cha kuwafanya waendelea kuwa katika biashara ya simu.