App ya Threads inayomilikiwa na kampuni ya Meta, wamiliki wa Facebook, Instagram na Whatsapp inatarajiwa kuanza kupatikana kwa watumiaji duniani kote Ijumaa ya wikiendi hii. Threads ni app inayolenga kuleta ushindani dhidi ya Twitter.
Mwezi wa Julai haujaanza vizuri kwa tajiri Elon Musk, amefanya maamuzi kadhaa ya ghafla kwenye mtandao wa Twitter yaliyosababisha watumiaji wengi kuanza kuangalia app zingine, huku app kama Truth Social ikipata maelfu ya watumiaji ndani ya muda mfupi kiasi cha kuathiri utendaji kazi wake.
Inaonekana kwenye kampuni ya Meta wakaona huu ni muda mzuri wa kuileta sokoni app yao inayolenga kuleta ushindani dhidi ya Twitter, nadhani wakiamini huu ni muda mzuri wa kupata watumiaji wapya ambao washachoshwa na kutotabirika kwa Musk.
Elon Musk ameleta mabadiliko gani?
Kwa muda mfupi, alizuia watu kuangalia tweets kama hawajaingia (Log in), kwa kipindi chote mtu ungeweza kwenda kutazama tweets mbalimbali na ata kutafuta bila ulazima wa kuwa umeingia.
Rate limits increasing soon to 8000 for verified, 800 for unverified & 400 for new unverified https://t.co/fuRcJLifTn
— Elon Musk (@elonmusk) July 1, 2023
Kuweka viwango vya uwezo wa kuona tweets, ukitaka kuona tweets nyingi kwa siku basi lazima uwe umejiunga katika huduma ya kulipia ya Twitter Blue. Watumiaji wa Twitter Blue kuweza kuona tweets 10,000 kwa siku, watumiaji wa kawaida kuona tweets 1,000 na huku watumiaji wapya wataona tweets 500 tuu.
Kwa nini? Kwa kiasi kikubwa watangazaji wengi wakubwa waliacha kununua matangazo kwenye mtandao huo baada ya mabadiliko mengi na hali ya kutofahamu kuhusu hali ya uendeshaji wa Twitter – hasa kwenye masuala ya usimamiaji wa maudhui (watangazaji wanataka uhakika matangazo yao hayatatokea kwenye maudhui yasiyofaa). Na sasa kumekuwa na utumiaji mkubwa wa data za mitandao ya kijamii unaofanywa na watengenezaji wa app za akili bandia (AI), kupitia njia hii ya upataji data wanatumia teknolojia za kupitia maelfu ya tweets kwa saa – hivi ni vitu vinavyodhidi kuongeza gharama upande wa Twitter. Hii inaonekana ni njia ya haraka ya kuwalazimisha watumiaji wa namna hii kuwalipa Twitter kwa matumizi ya aina hii.
Turudi kwenye Threads
Kupitia Threads Meta wanalenga kuchukua vyote vizuri kutoka Twitter, yaani mtandao wa kijamii unaoongozwa na mazungumzo kwa njia ya maneno. Ili kuweza kufanikiwa kwa haraka wamewawezesha watumiaji wote wa Instagram kuweza kuingia bila kutengeneza akaunti mpya. Watumiaji wa Instagram wataweza moja kwa moja kufuatilia akaunti zote wanazozifuatilia katika app ya Instagram, kwa kifupi app hii ni app dada kwa Instagram.
Changamoto
Tayari watu wanaona kama kuiamini app nyingine kutoka Meta itakuwa ni kuwapatia Meta data nyingi zaidi. Kumbuka kama wewe ni mtumiaji wa WhatsApp, Facebook, Messenger na Instagram, tayari Meta wanadata nyingi kuhusu wewe, kuwaongezea na app ya Threads inakuwa kuzidi kuwapa nguvu kubwa katika eneo la data. Hadi sasa kwenye appstore inaonekana app hiyo itahitaji haki za kuona data nyingi sana kuliko kawaida, na hii inaweza kuchangiwa na app hiyo kuunganishwa kimfumo na apps zingine za familia ya Meta.
Kwenye AppStore, ios, tayari app hiyo imewekwa kwenye orodha ya kutoka wikiendi hii ila kwa Google Playstore bado haipo, inawezekana ikaanza kupatikana kwa watumiaji wa iPhone kabla ya kuja pia kwa watumiaji wa Android.
No Comment! Be the first one.