Katika mwaka 2017 baada ya malalamiko ya watu ya muda mrefu, Apple walikubali ya kwamba huwa wanafanya iPhone za zamani kuwa nzito. Ila walisema wanafanya hivyo kwa sababu tofauti, si ya kulazimisha mauzo ya simu mpya.
Watu wengi walikuwa wanaamini Apple wanafanya hivyo ili kupandisha mauzo ya simu zao mpya.
Apple walivyojitokeza na kukubali ya kwamba huwa wanafanya simu hizo kupunguza ufanisi, walikuja na hoja ya kitofauti. Walisema wanafanya hivyo si kwa sababu ya kuongeza mauzo ya simu mpya bali ili kuhakikisha simu hizo za zamani zinaendelea kufanya kazi vizuri bila kuleta matatizo kwenye betri ambazo zinakuwa tayari zimeshaanza kuchoka.

Hivyo sababu yao ilikuwa wanafanya hivyo ili kuwalinda watumiaji wao dhidi ya milipuko ya betri inayoweza sababishwa na mahitaji makubwa mapya ya programu endeshaji za kisasa dhidi ya mabetri kwenye simu ambazo zimetoka miaka 2 au zaidi nyuma.
Chombo cha kuwalinda watumiaji na kusimamia ushindani wa kibiashara/bidhaa nchini Ufaransa, DGCCRF kimesema wanapiga faini Apple kwa kuwa uamuzi huo ulifanyika bila kuwataarifu wateja wao.
Uamuzi huu unaweza kuigwa kwenye vyombo vingine vya kisheria katika mataifa mengine na hivyo kusababisha malipo zaidi kutoka Apple kwenda vyombo vya kisheria katika mataifa mbalimbali hasa hasa ya Ulaya.
Je kuna njia ya kufanya simu isiathirike na suala hili ata kama imetoka miaka miwili au zaidi nyuma?

Apple wamesema programu endeshaji yao itapunguza ufanisi wa simu kwa kiasi flani kulingana na hali ya betri kwa wakati huo. Kuna watafiti ambao wamegundua ata kubadili betri tu la simu ambayo tayari imeanza kuwa nzito kunaongeza ufanisi kwa kiasi kikubwa kwenye simu husika.