Apple licha ya kuwa moja kati ya makampuni makubwa sana duniani, lakini bado inahangaika huku na kule katika kuhakikisha kwamba inajikuza zaidi.
Kwa sasa ripoti iliyopo ni kwamba kampuni hiyo nguli katika maswala ya kiteknolojia, ipo katika mazungumzo ya kulinunua kampuni la Lit Motors ambalo ni maarufu kwa kutengeneza vyombo vya usafiri wa matairi mawili maarufu kama piki piki.
Kampuni ya Lit Motors inatengeneza piki piki za teknolojia ya juu. Kwa haraka haraka piki piki hizi zina sura kama ya gari, na hazihitaji msaada wa aina yeyote katika kusimama/kuegeshwa (tumeshazoea piki piki za kawaida ni mpaka zishikiliwe au mtu ushushe – egemeo — stendi).
Kutokana na taarifa iliyotoka katika mtandao wa The New York Times ni kwamba kampuni la Apple tayari limeshaajiri wataalamu/mainjinia kadhaa kutoka katika kampuni la Lit Motors.
Lit Motors ina sifa kubwa katika teknolojia ya usafiri, imejipatia umaarufu mkubwa pale ilipotengeneza piki piki maarufu kwa jina la C-1. Kwa haraka haraka piki piki hii ina sura kama ya piki piki ya kawaida na magari ya kujiendesha yenyewe kutoka Google.
Hivi karibuni kampuni ya Apple imekua ikijihusisha sana na kutaka kununua makampuni mengine ambayo yamejikita katika Teknolojia ya usafiri. Jambo hili limetokea kwa sababu kampuni ya Apple ilifukuza wafanyakazi wake wengi katika kitengo chake cha magari.
Apple kwa kipindi cha muda mrefu imekua ikijianda katika kuleta teknolojia ya magari ya kujiendesha yenyewe, na hivyo iliandaa kitengo maalumu kinachoitwa Titan ambacho ndio kilikua kinasimamia shughuli zote za kuhakikisha wanaleta usafiri wa kujiendesha wenyewe.
Kuhusu mazungumzo hayo ya kuinunua kampuni ya Lit Motors pande zote mbili – Apple na Lit Motors – hazikuongelea swala hili.
Niadikie hapo chini sehemu ya comment, je unahisi kampuni la Apple litafanikiwa kulinunua kampuni la Lit Motors? Ningependa kusikia kutoka kwako.