Ripoti zinasema kuwa, makampuni ya kutengeneza simu janja duniani ya Apple na Samsung yameingia kwenye mjadala thabiti kushirikiana na makampuni ya mawasiliano ya simu kwa ajili ya kuleta laini mpya za simu. E-Simcard (Electronic simcard) zitakazomwezesha mtumiaji wa simu kubadili laini kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine bila kutoa laini yake.
Laini hizi zitasanifiwa miongoni mwa makampuni yote ya kutengeneza simu janja na kuingizwa katika simu zao, zitakazokuwa na mfumo unaofanana wa kukubali laini hizi.
Kampuni hizi kubwa mbili tayari zimeanza mazungumzo na kilele chake huenda ikawa mapema mwanzoni mwa mwaka 2016
Tofauti na laini za kawaida, laini hizi zinabadilika kirahisi zaidi kwa watumiaji wake ambapo, badala ya mtumiaji kuwa amesajiliwa kwenye kampuni moja tu (mfano kuwa na laini ya Vodacom tu, au line ya Tigo au Airtel tu), sasa mtumiaji ataweza kuchagua kampuni anayotaka kutumia kwa kubadili mtandao anaotaka bila kutoa laini iliyopo.
“Ni sawa kabisa na laini moja ya simu, kusapoti mitandao yote ya simu. Unachagua kutumia mtandao gani kwa kutumia mipangilio (settings) ya kwenye simu janja yako”. Alifafanua mchambuzi wa Smartphones Europe, Dr. Mark Denilson.
Mashirika makubwa ya mawasiliano ya simu ambayo yameingia kwenye mjadala wa kuleta laini hizi ni pamoja na AT&T, Deutsche Telekom, Etisalat, Hutchison Whampoa, Orange, Telefónica, na Vodafone.
“Kutokana na mashirika mengi kujiunga na mpango huu, kilichobaki ni kumalizia masuala ya kiufundi na kiutendaji yatakayotumika kuandaa SIM, mahususi kwa ajili ya vifaa vya wateja, huku mategemeo makubwa yakiwa kufikia mwaka 2016 zianze kutumika.” Ilisomekka sehemu ya taarifa iliyotolewa na The Financial Times kutoka GSMA, shirika kubwa kabisa duniani la mawasiliano ya simu. GSMA mwanzoni tayari wametengeneza E-Simcard kwa ajili ya vifaa vingine vinavyotumia laini, mfano taa za kuongozea magari barabarani.
Japokuwa mfumo huo mpya kutarajiwa kutangazwa punde, lakini huenda ukachukua mda kufika sokoni. Apple, Samsung na mshirika ya mawasiliano ya simu bado hayajamaliza Mazungumzo yatakayofikisha kilele cha mfumo huu mpya, The Financial Times lilieleza.
Tayari iPad Air 2 za Apple zinakuja na line zake spesheli zinazokuwezesha kubadili makampuni ya simu katika iPad yako bila ya kutoa laini kwa matumizi ya data pekee. The Financial Times linaripoti kuwa, hata hivyo mfumo huu mpya wa e-simcard hautabadili mfumo huu wa iPad Air 2 wa matumizi ya laini yake spesheli.
Kama mipango ikienda kama inavyotazamiwa, huenda teknolojia ya e-simcard ikazinduliwa sambamba na iPhone 7 mwishoni mwa mwaka 2016 katika maonyesho makubwa ya iPhone yanayofanyika Septemba kila mwaka
Kwa sisi watumiaji, mfumo huu utatunufaisha kwa kutuwezesha kuondoa usumbufu kwa kutoa na kuweka laini za simu ili kupunguza gharama za matumizi, kubadilisha laini ukisafiri nje ya nchi na Usalama na data na laini zako sasa utakuwa mkubwa zaidi.
Chanzo cha Makala haya ni mitandao ya Macworld, The Financial Times na iDownloadblog.
One Comment