Sasa unaweza kuzima uwezo wa USB katika iPhone. Apple wanazidi kuhakikisha kufanya simu ya iPhone kuwa moja ya simu salama zaidi duniani dhidi ya udukuzi au kuweza kufunguliwa bila ruhusa ya mtumiaji.

Apple walitofautiana na shirika la usalama na uchunguzi la Marekani la FBI baada ya kukataa kutoa msaada wowote kwa FBI kuwasaidia kufungua simu ya mtuhumiwa wa ugaidi. Kitendo hicho kiliwalazimisha FBI kutafuta msaada wa mashirika binafsi ya masuala ya udukuzi ili kuweza kuifungua simu hiyo.
FBI walifanikiwa kufungua simu hiyo kupitia kampuni moja ya nchini Israeli ambao wanatumia njia ya kompyuta ambayo ni siri mpaka sasa – lakini njia hiyo inahitaji kuunganisha kompyuta yao na simu husika kwa njia ya USB.
Katika toleo jipya la programu endeshaji la iOS 11.4.1 Apple wameleta kitu kipya cha usalama katika programu endeshaji hiyo inayofanya suala la kuweza kuchezea programu endeshaji hiyo kwa njia ya USB kuwa ngumu zaidi.
Wameleta uwezo ambao ndani ya Settings mtumiaji anaweza kuzima uwezo wa eneo la USB kutumika kwa kazi yeyote zaidi ya kuchaji tuu. Hii inamaanisha eneo la USB linashindwa kupewa ruhusa ya kuwasiliana na sehemu yeyote ya programu endeshaji ya iOS zaidi ya kuchaji tuu.
Sehemu ya kuzima na kuwasha uwezo wa USB kwa simu za iPhone unapatikana kwenye Settings -> Touch ID & Passcode -> USB Accessories.
Baada ya saa moja tokea simu ilikuwa imekuwa ‘unlocked’ moja kwa moja uwezo wa kutumia au kutambua USB unajizima. Kuruhusu tena inabidi mtu ai’unlock simu na kisha aende kuwasha uwezo huo tena.
