Kampuni ya Apple yatishia kuondoa huduma za Facetime na iMessage nchini Uingereza kwa watumiaji wa vifaa vyake kama vile iPhone, iPad na Macbook wa nchini humo.
Apple wametoa maelezo hayo kama sehemu yao ya kupinga sheria mpya na maboresho ya sheria zinazosimamia masuala ya usalama na ulinzi wa data za watu mtandaoni nchini Uingereza. Sheria hizo zinalenga kulazimisha makampuni kuchukua hatua kwa haraka katika kuondoa na kufuta maudhui yasiyo sahihi, na kwa yale yatakayochelewa kutakuwa na hatua kali za adhabu zinazoweza husisha ulipaji wa faini.
Katika mapendekezo ya maboresho ya sheria ya Mamlaka ya Uchunguzi (Investigatory Powers Act 2016) wizara ya mambo ya ndani ya nchini humo inapewa nguvu kubwa katika kuchunguza na ata kukataa maboresho ya teknolojia ya ulinzi na usalama ya kidigitali ya ‘encryption’ (Fahamu zaidi kuhusu encryption hapa – Teknokona / Encryption) . Apple inapinga maboresho haya ikisema teknolojia hiyo na maboresho ya aina yeyote yanayofanywa na kampuni hiyo yanalenga kuwalinda watumiaji wake.
Uwepo wa mapendekezo ya maboresho hayo yanaonesha Serikali inataka kuwa na nguvu ya kukataa maboresho ambayo yafanya ata vyombo vyake vya kiuchunguzi kushindwa kuingilia kati au kupata data za wale wanaowachunguza – kiufupi wanataka kuwa na uwezo wa kuwa na njia mpabadala ya kuishinda teknolojia hiyo.
Kwa muda mrefu mataifa mengi ya Magharibi yamekuwa yakirusha makombora ya mambo kama haya kufanywa na serikali ya China, hivyo kwa wengi mapendekezo ya sheria ya kuvipa vyombo vya usalama nafasi kubwa katika kuingilia teknolojia za usalama wa data na mawasiliano ya watu hayakutegemewa kufanywa na serikali ya Uingereza.
Apple wameendelea kuishauri serikali hiyo kutoendelea na maboresho hayo ya sheria, wakisema badala ya kuongeza ulinzi na usalama kwa watumiaji jambo hilo litakuwa linarudisha nyuma juhudi zake. Apple wamesema Serikali hiyo ifahamu ikilazimisha jambo basi ata mataifa mengine pia muda si mrefu serikali zao zitataka nazo kuweza kuwa na uwezo huo – hivyo kuzidi kutishia usalama wa watumiaji wake wa aina mbalimbali, hii ikiwa ni pamoja na wanahabari nyeti na wapinzani wa kisiasa wa watu walio madarakani.
Msimamo wa mwisho wa Apple ni kwamba hawataachia kuendelea kuishauri serikali kutoendelea na zoezi la kupeleka mswada huo wa sheria bungeni, ila kama sheria zitapita kama zilivyo kwa sasa na kuanza kutumika hapo mwakani basi Apple kuliko kukubali kushusha ulinzi na usalama wa huduma zake ataona ni bora kuziondoa kwa watumiaji wa Uingereza.
Wengi wanaona sheria hiyo inaweza ikawaathiri watu wengi sana na hivyo kuwapa sababu ya kuanza kuongea na wawakilishi wao bungeni ili kupinga mapendekezo hayo ya sheria. Data za tafiti za mwaka 2022 (Statista), zinaonesha Apple anashikilia soko la Uingereza la simu kwa asilimia 50%. Watumiaji wa iPhone wakiwa zaidi ya milioni 19.7, huku kwa ujumla pamoja na watumiaji wa vifaa vingine vyote vya familia ya Apple idadi ikipanda hadi milioni 29.2.
Kama maboresho na mapendekezo ya sheria mpya yakipita kama yalivyo, tunaweza kuona Apple akifanya uamuzi utakaowaumiza maelfu wa wateja wao.
No Comment! Be the first one.