Kampuni la Blackberry limejikuta likijikongoja baada ya kutofikia malengo yake ya mauzo ya simu janja zake licha ya kwamba wana simu mpya sokoni ambazo zinatumia programu endeshaji ya Android.
Kama unakumbuka vizuri kuna kipindi Blackberry ndio ilikua mfalme wa simu janja, kuna mambo yakajitokeza na hatimaye soko likachukuliwa na wengine kama vile Google pamoja na Apple.
Ukiachana na hayo kampuni likajipanga kurudi na ili kuhakikisha linabaki katika soko likajiwekea misingi ya kuifikia. Ili kubaki katika soko kampuni lilihitaji liuze angalau simu zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 566.
Licha ya simu yake maarufu ijulikanayo kama BlackBerry Priv kuwa katika soko na kuuzwa kwa kiasi cha juuu (dola za kimarekani 699) bado namba hiyo – dola milioni 566 za kimareknai — haijapatikana
Ripoti yake ya vitabu vyake vya mahesabu vya miezi mitatu iliyoishia februari 29 vinaonyesha mapato ya aina mbili. Ya kwanza ni dola milioni 487 ambazo zinatokana na mapato ambayo haya endani na kanuni za uhasibu (Non GAAP) na ya pili ni dola 464 za kimarekani ambazo zinatokana na mapato ambayo yanaendana na kanuni na taratibu zote za uhasibu (GAAP). Ukiangalia namba hizi za mapato ni tofauti kabisa na zile zilizotabiria mara ya kwanza na wataalamu ambazo zilikuwa dola 566 za kimarekani.
Simu ya Blackberry Priv inatumia programu endeshaji maarufu kutoka Google, Android na pia simu hiyo inasifika kuwa na ulinzi wa hali ya juu ambao simu za BlackBerry zimekuwa zikisifika nao kwa muda mrefu sasa. Cha kushangaza ni kwamba simu hii imepokea sifa nyingi sana tena zile nzuri nzuri kutoka kwa wataalamu wa simu lakini zimekuwa na mauzo madogo sana.
Bw. Chen ambaye ndio mkurugenzi wa BlackBerry amelalamikia mauzo madogo kwa simu za bei kubwa kwa ujumla na maongezi na makubaliano ambayo yamechukua muda mrefu kutoka kwa watoaji huduma za mitandao (kama vile Sprint, Verizon n.k)
Bw. Chen bado anaamini anaweza kubakia katika soko la simu kwa mkakati huu: kwa wakati huu ana mpango wa kuweka sokoni simu ya gharama ndogo ili aishinde kimauzo ile ya gharama kubwa (priv) katika soko. Pia ataongeza usambazaji na itawabidi wauze simu angalau milioni 3 ili wafikie katika eneo ambao hawatapata faida wala hasara.
Inamaanisha kuwa kama mauzo ya simu yakizidi simu milioni 3 basi kampuni litaanza kulamba faida. Katika simu hizo milioni 3 kila simu ikiuzwa kwa angalau dola za kimarekani 300 basi kampuni litajihakikishia kubaki katika soko la simu kama ikishindikana huo ndio utakuwa mwisho wa simu za Blackberry
Kama kampuni itaachana na biashara ya simu, itaendelea na biashara yake ambayo inaiweza vilivyo. Yaani biashara yake ya kutengeneza ‘Software’. Aina hii ya biashara inaonyesha faida kubwa kwa kampuni. Biashara hii iliipatia kampuni faida ya dola milioni 500 za kimarekani kwa mwaka wa hesabu uliopita wa kampuni hiyo.
Kwa sasa kampuni ina mpango wa kukuza kitengo cha biashara ya ‘software’ katika kampuni hilo kwa asilimia 30.
Kwa mtazamo wangu naona kampuni hili inabidi lijitahidi ili mradi lisipotee katika soko la simu janja. Kumbuka kama kukiwa na makampuni mengi yanayotengeneza simu janja inamaanisha kutakuwa na ushindani wa hali ya juu. Ushindani mkubwa utayapa ‘tumbo joto’ makampuni makubwa. Ikitokea hivyo basi watu wataanza kupata simu janja zenye uwezo wa juu kwa kiasi kidogo cha pesa