Biashara ya utengenezaji na uuzaji wa simu za Honor imeuzwa na kampuni ya Huawei. Kuanzia sasa simu zinazobeba jina hilo hazitatengenezwa wala kuuzwa na kampuni ya Huawei.
Katika uamuzi unaonekana kuja kutokana na madhara ya vikwazo walivyowekewa na serikali ya Marekani, kampuni ya Huawei imeamua kuuza biashara nzima ya utengenezaji na uuzaji wa simu zake maarufu za jina Honor kwenda kwa kampuni nyingine inayomilikiwa na wafanyabiashara mbalimbali nchini China.

Kutokana na vikwazo vya serikali ya Marekani tayari simu hizo zilionekana zitaathirika sana kimauzo na pia biashara hiyo ilianza kuathirika katika upatikanaji wa vipuri vya utengenezaji wa simu.
Kundi la wafanyabiashara waliokuwa wananufuika kutokana na uwepo wa simu hizi yaani wamiliki wa maduka mbalimbali na wale waliokuwa wanawauzia vipuri mbalimbali Huawei wamejumuika kwa pamoja na kutengeneza kampuni nyingine na kuiomba Huawei kuwauzia ili wasiathirike na madhara ya vikwazo vya Marekani.

Tokea mwanzoni biashara ya simu za Honor ndani ya kampuni ya Huawei zilikuwa zikijitegemea kwenye utengenezaji na uendeshaji wa simu zinazobeba jina la Honor. Simu hizi zimekuwa zikilenga vijana, zikiwa ni simu za bei nafuu ila zenye muonakano mzuri.
Inasemakana Huawei wameuza biashara hiyo kwa takribani Dola Bilioni 15.2 za Kimarekani, yaani zaidi ya Sh. Trilioni 35 za Kitanzania.
No Comment! Be the first one.