Katika hali inayoonekana ni maamuzi magumu, kampuni maarufu ya BlackBerry kupitia mkurugenzi wake imekiri kufanya uamuzi wa kuja na simu zinazotumia programu endeshaji ya Android.
Kwa miaka mingi simu za BlackBerry zimekuwa zikitumia programu endeshaji ya BlackBerry OS na tokea ujio wa simu za iPhone na ukuaji wa utumiaji wa simu za Android, BlackBerry imejikuta ikisaulika na watengenezaji wa apps. Kutokuwepo kwa apps nyingi maarufu kumechangia kwa kiasi kikubwa simu za kampuni hiyo kufanya vibaya sokoni kwa muda mrefu sasa.
“Naenda kuondoa suala la upatikanaji wa apps kama sababu ya kutonununua simu zetu. Tutaangalia matokeo yake.” – Alisema Bwana Chen
Simu ya kwanza itakayotumia Android kutoka kwa BlackBerry itafahamika kwa jina la Priv.
Soko la apps la BlackBerry lina takribani apps laki moja hivi wakati soko la apps la Google Play na la Apple (app store) yanazaidi ya apps milioni moja kila moja.
Uamuzi wa kuingia kwenye utengenezaji wa simu za Android ndio uamuzi wa mwisho katika jitahada za kampuni hiyo kuokoa biashara yake ya utengenezaji na uuzaji wa simu. Katika miaka ya karibuni kampuni hiyo imeweka jitihada zaidi katika kuwekeza katika teknolojia zaidi baada ya kuona mapato katika biashara ya simu yakiporomoka. Bwana Chen amesema ingawa wanaleta simu za Android bado wataendelea kuleta simu zenye programu endeshaji yake ya BlackBerry OS.
Je umekuwa mpenzi wa simu za BlackBerry? Unaona uamuzi huu ni mzuri?
No Comment! Be the first one.