Bunge la Tanzania kupitia spika wake Job Ndugai limetangaza kuendesha shughuli zake za vikao kwa njia ya mtandao kwa wabunge wote.
Spika Job Ndugai amesema Bunge litasitisha kutoa karatasi zinazoonesha orodha ya vikao vya shughuli za bunge na badala yake taarifa zote zitatumwa kwa wabunge kwa njia ya mtandao.
“Nataka kuwaambia wabunge kuwa karatasi hizi ambazo tunazitumia kuonesha orodha ya shughuli za Bunge, leo (03 Septemba 2019) ndio mwisho kuingia humu ndani. Kwa maana nyingine tutakuwa tunawatumia kwa njia ya mtandao, sasa waheshimiwa wabunge naomba mhakikishe mnaweka namba zenu za simu vizuri, barua pepe (E mail) vizuri na lengo la kuhakikisha meza za wabunge haikai na makaratasi na badala yake zinakuwa nyeupe kabisa”, alisema spika.

Hatua hii inakuja baada ya ushauri ili Bunge letu liwe Bunge Mtandao. Ni kwamba wabunge watalazimika aidha kuwa na Simu Janja, Laptop, au Tablet/iPad pamoja na kuwa na E mail ili kuweza kutumiwa taarifa zote za kibunge.