Kukamilika kwa kiwanda cha Chip cha Huawei cha kwanza nchini China ni ishara kubwa ya uamuzi wao wa kuhakikisha wanajitegemea katika teknolojia muhimu za utengenezaji simu.

Chip / Chipset ni nini?
Kwenye simu chipset zinatambulika kama system-on-chip. Kwenye kompyuta na simu chip ni kifaa kidogo kinachosimamia ufanyaji kazi wa vifaa vingine kama vile unafanyaji kazi wa USB, mifumo ya sauti na sehemu zingine za kompyuta. Chip mbili au zaidi zikiunganishwa kwa pamoja ndio zinatengeneza chipset. Vifaa kama simu vimechangia sana ukuaji wa teknolojia ya chipset zenye nguvu na ufanisi mkubwa.
Huawei kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia chipset za Snapdragon na za kwao zilizokuwa zimebeba jina la Kirin. Fahamu zaidi kuhusu chip na chipset kwa kusoma makala yetu hapa – Chipset ni nini?
Kama Huawei tayari wanaprosesa zao za Kirin, kwa nini hichi kiwanda kinaitwa kiwanda chao cha kwanza cha utengenezaji chip?
Ingawa Huawei walibuni prosesa zao za Kirin ambazo wamezitumia katika baadhi ya simu hadi sasa, prosesa hizo zinatengenezwa na kampuni ya utengenezaji chip ya TSMC ya nchini Taiwani. Kampuni ya TSMC haiwezi tena kuendelea kuwatengenezea Huawei chip kwa kuwa wanatumia vifaa na teknolojia za kimarekani katika utengenezaji chip. Vikwazo vya Marekani vimezuia kampuni mbalimbali duniani kuweza kuipatia kampuni ya Huawei vipuri vinavyotumia teknolojia ya Marekani kwa namna yeyote ile.

Wengi wanategemea kupitia kiwanda chake cha chip basi Huawei atakuja na jina jipya kabisa kwa ajili ya chip zitakazokuwa zinatengenezwa katika kiwanda hichi. Wakati huo huo tayari kiwanda cha pili cha utengenezaji chip kipo katika hatua za mwisho katika jiji la Shanghai.
Kwa kuanzia chip za kwanza zitatoka mwakani zikiwa na ukubwa wa nanomita 45, wanategemea hadi kufikia mwaka 2022 wataweza kupunguza ukubwa na kufikia nanomita 28. Chip bado ni kubwa sana ukilinganisha na zingine kutoka makampuni mengine kama vile Snapdragon na wengine, ambazo kwa sasa zimekuwa ndogo zikiwa hadi na ukubwa wa nanomita 5. Kumbuka kipimo cha nanomita ni kidogo sana, sentimeta 1 ni sawa nanomita 10,000,000.
Wakati huo huo Huawei wamesisitiza ujio wa simu na vifaa vingine janja vikiwa vinatumia programu endeshaji yao ya Harmony OS. Tutegemee kwa mwaka 2020 kuona utumiaji zaidi wa programu endeshaji hii ili kuepukana na vikwazo vya Marekani katika utumiaji wa toleo la Android linalokuja na huduma za Google Play na huduma zingine muhimu za Google kupitia Android.
No Comment! Be the first one.