Je ushawahi jiuliza chipset ni nini kwenye simu n.k.? Chipset ni moja ya kiungo muhimu kwenye simu janja yako. Ni kitu kinachowezesha simu yako iweze kufanya kazi zake za kitofauti tofauti kwa ufanisi mkubwa – bila kutumia chaji nyingi sana, kutochukua nafasi kubwa ndani ya utengenezaji wa simu na faida nyingine nyingi.
Kihistoria chip zilianza kutumika kwenye kompyuta, na kipindi ilikuwa kifaa hichi kimoja yaani chip kinabeba kazi moja husika tuu. Na hivyo ili kutengeneza kompyuta moja ilihitaji utumiaji wa chip kadhaa ili kuwezesha kompyuta husika kuwa na uwezo wa kufanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja.
Utendaji wa kazi za aina mbili au zaidi ukiwezeshwa katika chip moja basi chip hiyo ndio inabeba jina la chipset. Teknolojia ya chipset imefanikiwa zaidi kwenye simu janja, kwa sababu imeruhusu simu kuweza kuwa na uwezo wa kufanya kazi nyingi na huku zikiwa na ukubwa mdogo – kwa kuwa chipset ni kama vile ubongo mzima unaounganisha uwezo wa kiutendaji wa simu.
Chipset ya simu ndio inabeba uwezo wa simu husika kuweza kuvitambua na kutumia teknolojia mbalimbali kama vile za mawasiliano ambazo vipuli vyake vimeunganishwa kwenye simu husika. Simu itaweza kuvitambua vifaa na teknolojia hizo za ziada na kuzitumia kupitia utendaji kazi wa chipset yake.
Makampuni yanayoongoza kwa utengenezaji wa chip kwenye biashara ya vipuri vya simu ni:
- Qualcomm — Hawa ndio wanashikilia soko la chip za simu. Chipsets zao maarufu zinabeba jina la Snapdragon na zinatumika kwenye simu nyingi zaidi za Android.
- MediaTek — Hizi ni chipset za gharama nafuu ambazo zinatumika sana kwa simu janja za bei ya kati (Mid range). Ni maarufu sana kwa makampuni yanayotengeneza simu ambazo ni za bei nafuu lakini zenye hadhi ya kati. Kampuni ya MediaTek inashika nafasi ya pili kwenye soko la chipset.
- Huawei — Huawei wanatengeneza chipset zao zinazobeba jina la HiSilicon Kirin. Hizi ni chip za ubora wa juu na zenye nguvu sana, zinatumika kwenye baadhi ya simu za Huawei na kwa iliyokubwa brand yao ya simu za Honor. Kwa sasa wameuza biashara ya simu za Honor.
- Samsung — Samsung pia wanatengeneza chipset zao zenye nguvu na zinazotumika kwenye simu zao zenye uwezo mkubwa. Chipset zao zinafahamika kwa jina la Exynos, na tayari chipset hizo zimeshatumiwa na makampuni mengine kama vile kampuni ya Vivo.
- Apple — Apple pia wanatengeneza chip za ubora wa juu ila tofauti na wengine wote ni kwamba chipset zao zinatumika kwenye simu zao tuu. Na hivi karibuni wameweza kutumia teknolojia yao ya chipset za kwenye simu katika utengenezaji wa chipset kwa ajili ya kutumika kwenye laptop zao za Macbook, chipset hizo zimeonesha ufanisi wa hali ya juu kuzizidi chips za Intel walizokuwa wanazitegemea kwenye kompyuta zao.
Aina ya Chipsets zinazotumika kwenye simu kulingana na ubora na uwezo wa simu:
Simu za bei nafuu (Bei za chini Tsh 150,000/= – Tsh 400,000/=
- Chipset za Snapdragon na MediaTek.
- Huawei – HiSilicon Kirin
- Samsung – Exynos
Snapdragon na MediaTek wote wana chipset spesheli za bei nafuu kwa ajili ya kutumika kwenye simu za bei ya kawaida. Wote kwa pamoja wamelishikilia soko la simu za bei nafuu.
Simu za bei ya kati (Midrange – Tsh 350,000/= – Tsh 950,000/=)
- Huawei – HiSilicon Kirin chips
- MediaTek
- Snapdragon
- Samsung – Exynos
- Chip za Apple
Chipset za MediaTek zinasifa nzuri katika utumiaji mdogo wa chaji lakini pia zina uwezo mdogo katika ufanisi wa uchezaji magemu ukilinganisha na zile za familia ya Snapdragon au zile za Apple zinazotumika kwenye simu za iPhone.
Simu za Bei ya Juu (Premium Range – Tsh 800,000/= – Tsh 2,500,000/=)
- Chip za Apple
- Chipsets za Snapdragon kutoka Qualcomm
- Chip za HiSilicon Kirin kutoka Huawei
- Chip za Exynos kutoka Samsung
Leo tunategemea utakuwa umeelewa zaidi kuhusu masuala yanayohusu chip na chipset zinazotumika kwenye simu janja. Je ni kipi kingine ungependa kufahamu zaidi kuhusu simu au laptop? Tuulize kwenye comments.
No Comment! Be the first one.