Google Chrome inaweza kukupa taarifa kutoka mitandao uipendayo, kwa mfano, umepata rafiki mpya wa Facebook. Firefox iko mbioni kukuwezesha kutumia ‘extensions’ za Chrome na Opera. Katika kipindi ambacho, njia kuu ya watu kuingia mtandaoni ni vivinjari, ni jambo la muhimu kukuletea maboresho ya programu hizo ili kukuwezesha kufaidi zaidi teknolojia.
‘Chrome Notifications’ na ‘Chrome Custom Tabs’
Kwa muda mrefu, Chrome imekuwa ikitenganisha kila ‘tab’ (uwanja wa kurasa unayofungua) kuwa prosesi tofauti ili kuongeza usalama wa kivinjari. Imejulikana kwamba ukitenganisha tabs, unapunguza wigo wa mdukuzi kushambulia kifaa chako kupitia intaneti. Jambo lililotokana filosofia hiyo ni uwezo wa wa tab mahsusi kwa huduma fulani za intaneti. Tab hizo zina uwezo wa kuwa na tabia za kufanana na app ya hiyo huduma unayotaka. Kwa mfano, ukifungua Pinterest kwenye Chrome, inaweza kukupa chaguzo (menu) ya kuhifadhi picha papo kwa hapo au Ku-Pin, kama vile ilivyo kwa app ya Pinterest kwa Androidi! Pengine jambo kubwa zaidi ni kwamba ‘Custom tabs’ zitafaya tovuti ya huduma husika kufunguka kwa haraka zaidi.
Chrome Notifications: Katika hatua nyingine, Chrome ya sasa inakuwezesha kupata taarifa kutoka kwa huduma upendazo kama Facebook na Twitter bila hata ya kuwa na app zake!
Hii ni muhimu sana kutambua, hasa kama una simu yenye uwezo mdogo kwani itapunguza ulazima wa kuwa na app nyingi kwenye simu yako. Chrome notifications ni habari njema pia kwa wasukaji wa programu kwani itakuwa sio lazima sana kwa tovuti au huduma fulani rahisi kuwa na app yake ya Android. Kwa sasa, huduma zinazotumia uwezo huu ni chache na ni zile kubwa kwenye mtandao kama, eBay, Facebook, Pinterest, Vice News, na Product Hunt.
Chrome Notifications huanza kujionesha unapokubali kuingia (sign-in) kwenye huduma fulani kwa mara ya kwanza. Chrome itakuuliza kama utapenda kupata taarifa kutoka kwenye huduma hiyo. Pamoja na hivyo, unaweza kuweka njia ya mkato kufikia huduma yako husika kwenye skrini ya mwanzo kwenye simu ili kuifikia haraka.
Kuweza kutumia huduma za Chrome Notifications na Chrome Custom Tabs, itakubidi usasishe kivinjari chako cha Chrome kwa ajili ya Android. Kwa sasa, Google hawajaleta vipengele hivi kwenye vifaa vya Apple.
Firefox kutumia ‘Extensions’ za Chrome na Opera
Mabadiliko makubwa yamekuja kwenye kivinjari cha Firefox hivi karibuni ambayo yatafanya visaidizi (add-ons) kubadilika tabia. Mozilla wametoa ‘API’ iitwayo WebExtensions inayofanana na mfumo wa Chrome na Opera, ili kuwezesha visaidizi kutumika kati ya vivinjari tofauti.
Katika mabadiliko hayo, kuanzia toleo jipya la Firefox wanaloliita ‘Electrolysis’, kivinjari cha Firefox kitagawanya ‘tabs’ kuwa prosesi tofauti ili kupunguza madhara ya kivinjari chako kikipatwa na programu hatarishi.
Habari kwa wasukaji wa programu (developers) ni kwamba inabidi wabadilishe visaidizi walivyotengeneza ili viweze kufanya kazi na Firefox, kwani kuanzia September 22, Firefox wataanza kuhakiki programu na kuzikubali kwenye soko lao la visaidizi.
Habari hii inatuusu pia watumiaji wa kawaida kwani inatuweka kwenye wakati mzuri wa kuchagua kivinjari chochote bila ya hofu ya kukosa visaidizi muhimu.
Hizi habari zote, za Chrome na Firefox ni nzuri kwa watumiaji wa intaneti, hasa kwenye simu za mkononi. Juu ya yote la Firefox kuzidisha juhudi zake na kufanikiwa kutenganisha ‘tabs’ kuwa prosesi tofauti ni la muhimu zaidi. Limesubiriwa sana. Kufuatia hili, usalama wa Firefox umeimarika, ingawa itasababisha Firefox kuwa nzito zaidi. Ijulikane kwamba suala hili si geni kwani tayari limekwishafanyika kwa namna tofauti kwenye vivinjari vingine vikubwa vya Chrome (tangu 2008) na Ms. internet Explorer.
Chanzo: theNextWeb, theVerge
No Comment! Be the first one.