Elon Musk na Twitter zimekuwa moja ya mada maarufu sana katika miezi hii michache. Uamuzi wa tajiri namba moja kununua mtandao wa Twitter umekuja na changamoto mbalimbali – kuanzia siku aliyosema kwamba ana nia hiyo, jinsi ambavyo baadae akataka kubadili uamuzi, kitu ambacho kilisababisha uongozi wa Twitter kumfungulia mashtaka ya kulazimisha mauzo kukamilika. Baada ya kuona mambo magumu aliamua kukamilisha ununuzi huo. Sasa baada ya sakata lote la ununuaji kukamilika, je ni nini kinafuata?
Kazi ya Ujenzi wa timu yake mpya
Haina ubishi kuna asilimia kubwa ya wafanyakazi wa mtandao huo wa kijamii ambao si mashabiki sana wa mitazamo ya Bwana Musk, tokea aoneshe nia ya kuununua mtandao huo tayari wafanyakazi wengi walianza kuonesha kutopendezwa na jambo hilo. Hali ilikuwa mbaya kiasi cha uongozi wa kampuni hiyo kuweka baadhi ya vikwazo katika usimamiaji wa data na teknolojia muhimu zinazoendesha mtandao huo wa kijamii ili kuepusha vitendo vya kihujumu ambavyo vingewezwa kufanywa na wale ambao hawapendezwi na ujio wa Elon Musk.
Na ni kutokana na hili pamoja na nia ya kupunguza gharama za uendeshaji Bwana Elon Musk na uongozi wake tayari wametoa taarifa kwa wafanyakazi wote juu ya uamuzi wa uongozi wake kupunguza zaidi ya nusu ya wafanyakazi wa kampuni hiyo. Walitumiwa ujumbe wa barua pepe wa ghafla ukiwataka ata wasifike ofisini, wabaki nyumbani wakiwa wanasubiri kuhusu taarifa juu ya maamuzi ya ajira zao. Muda huo huo wenye kompyuta za ofisi walijikuta hawawezi tena kuingia kwenye akaunti zao. Inakadiriwa takribani wafanyakazi 3,700 wapo katika hatari ya kupoteza kazi.
Tayari kuna kundi la wafanyakazi ambalo limefungua kesi ya kupinga kufukuzwa kazi ghafla bila kupewa muda wa kisheria wa siku 60.
Mara tuu ya manunuzi ya mtandao huo kukamilika kisheria Bwana Elon Musk alimfukuza kazi Mkurugenzi Mkuu Bwana Parag Agrawal pamoja na vigogo wengine kadhaa ikiwa ni pamoja na wale waliokuwa kwenye eneo la sheria na maamuzi ya kusimamisha (ban) akaunti za watumiaji wa mtandao huo.
Uthibitisho wa Akaunti (Blue Tick) kuuzwa kwa gharama ya $8 kwa mwezi
Kama ilivyo kwenye mitandao mingine ya kijamii kama vile Instagram na Facebook, akaunti za watu muhimu au mashuhuri huwa zinapatiwa uthibitisho maalum na kuweka alama ya vema maarufu kama blue tick. Kwa sasa utaratibu uliopo ulikuwa unalalamikiwa kwa kuwa ulikuwa unaweza kuchukua muda mrefu sana, na usio na uwazi katika hatua zake. Hivyo kuna akaunti nyingi za makampuni na watu mashuhuri ambao hawakufanikiwa kupata uthibitisho wa akaunti zao.
Bwana Elon Musk ameona jambo hili linaweza kutumika kama chanzo cha mapato kwa mtandao huo wa kijamii amabao kwa muda mrefu umekuwa unapata changamoto ya kutengeneza faida.
Vitu muhimu kwenye mpango wa Elon Musk na Huduma ya Uthibitisho wa Akaunti
- Kuweza kuwa na hadhi ya blue tick – mtumiaji atalipa Twitter $8 (Takribani Tsh 16,000/=) kila mwezi
- Kiwango cha dola 8 ni kwa mataifa ya juu kiuchumi, kwa mataifa mengine gharama itashuka kulingana na hali ya uchumi ya taifa husika
- Faida za kupewa kipaumbele kwenye baadhi ya maeneo ya kwenye mtandao huo; mfano majibu yako kwenye mazungumzo kuwekwa juu zaidi ukilinganisha na ya wengine, akaunti yako kupewa kiupaumbele cha kuorodheshwa juu zaidi katika utafutaji (search) kwenye mtandao huo nk.
- Akaunti yake kutowekwa matangazo mengi zaidi ukilinganisha na ile ya mtumiaji wa kawaida kwenye Timeline
- Uwezo wa kupandisha (upload) video na sauti zenye muda mrefu kuliko sasa
Ingawa kuna wengi wanaosema hawatalipia huduma kama hiyo ila inaonekana bado kwa wale ambao matumizi yao ya mtandao huo wa kijamii ni ya kibiashara zaidi watatumia huduma hiyo.
Mauzo ya matangazo yaporomoka
Makampuni mengi yamesimamisha ununuaji wa matangazo kupitia mtandao huo wa kijamii kwa muda huku wakitaka kuona kama mabadiliko ya uongozi hayataathiri sifa na hadhi ya mtandao huo wa kijamii. Bwana Elon Musk kupitia akaunti yake ya Twitter alitoa lawama kwa wale wanaopinga ununuaji wake wa Twitter akiwatuhumu kwamba kuporomoka huko kwa mauzo kumesababishwa na kampeni ya chuki dhidi yake.
Mbele mambo yatakuwa salama?
Elon Musk si mtu rahisi katika kutabili maamuzi au atakachosema, ila hakuna ubishi ya kwamba ni mmoja kati ya wafanyabiashara wazuri katika kunyanyua kampuni ambazo hazikuwa zikifanya vizuri. Na haitakuwa mara ya kwanza anafanya jambo ambalo ni la kitofauti, kumbuka wakati anaanzisha kampuni ya roketi za anga za juu, Space X, maono yake ya mafanikio ya kutengeneza roketi zinazotua salama bila kuharibika na kisha kuzitumia tena (reusable) lilionekana ni kichekesho. Kuna wana anga wabobezi walisema haielewi sekta hiyo na jambo lake halitafanikiwa – ila wote hawa amekuja kuwaumbua.
No Comment! Be the first one.