Elon Musk vs Mark Zuckerberg kuzichapa ulingoni. Moja ya habari iliyosambaa sana wiki iliyopita ni ya kuhusu boss wa Twitter, Elon Musk kuzichapa na Mark Zuckerberg, muanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya Meta (wamiliki wa Facebook, WhatsApp na Instagram).
Jambo hilo lilianza kama utani baada ya taarifa za chini chini kuonesha kampuni ya Meta inafanyia kazi ujio wa mtandao wa kijamii utakaoshindana na Twitter, unaokwenda kwa jina la ndani kwa sasa la Threads.
Inasemakana Meta wanataka kutumia nguvu kubwa ya watumiaji wao wa mtandao kama Instagram kuwafanya pia wawe watumiaji wa mtandao wa kijamii wa Threads bila kuathiri marafiki ambao tayari wanao – yaani unaingia (login) kwenye mtandao huu kwa kutumia taarifa zako zile zile za Instagram.
Lengo kuu ni kuja na mtandao wa kijamii ambao unafanana kabisa na mfumo wa Twitter – wa kuwa wa maneno zaidi ‘tweets’.
Ni tofauti gani kubwa ipo kati ya Musk na Zuckerberg
Mitandao ya kijamii: Musk amekuwa mkosoaji mkubwa wa majukwaa ya Meta, haswa Facebook, ambayo anaituhumu kwa kueneza habari potofu, kudhuru demokrasia – kwa maamuzi kama ya kuzuia akaunti na maoni ya mlengo wa kushoto nchini Marekani (Republicans), na kuingilia faragha. Na sasa Meta wanakuja na mtandao wa kushindana na Twitter.
AI – Akili Bandia: Musk na Zuckerberg wana maoni tofauti sana juu ya uwezo na hatari za teknolojia ya akili bandia (AI). Musk ni mtetezi mashuhuri wa kudhibiti AI na kuhakikisha maendeleo yake ya yanaendana na kulinda na usalama wa wanadamu, kwani anaogopa kuwa AI isiyodhibitiwa inaweza kuwa tishio la kiuhai kwa binadamu. Zuckerberg ni mwenye matumaini zaidi juu ya AI na faida zake kwa jamii, na amedai kuwa onyo la Musk ni “hasi sana” na “linaonesha uelewa mdogo kuhusu teknolojia hiyo”.
Turudi kwenye pambano
Kutokana na habari za ujio wa Threads, Musk alitweet kwa kejeli kwamba alikuwa na hakika “Dunia haiwezi kusubiri kuwa chini ya kidole cha Zuck peke yake”, na akaongeza kuwa alikuwa “tayari kwa pambano spesheli la kwenye kizimba ikiwa Zuckerberg atakubali”.
Zuckerberg alijibu kwa kutuma skrini ya tweet ya Musk kwenye akaunti yake ya Instagram na kichwa cha habari “Nitumie eneo”. Msemo huu unatumiwa sana na wapiganaji wa mashindano ya UFC kujibu pambano lililotakiwa na wapinzani wao. Musk alijibu “Vegas Octagon”.
Mabishano haya mafupi yaliienea kwenye mitandao ya kijamii, na watumiaji wengi wakionesha nia ya kuona jinsi matajiri hawa wakubwa wa sekta ya juu ya teknolojia wakipigana. Wengine pia walitengeneza vichekesho, na mabango ya utani kuhusu mapigano haya.
Sehemu kubwa ya utani ni kwamba Bwana Musk anaweza chezea kichapo kutoka kwa Mark kwa kuwa bosi wa Facebook amepitia mafunzo ya mchezo wa Jiu-Jitsu na ameshashinda mapambano kadhaa.
No Comment! Be the first one.