Kampuni la Facebook kwa ujumla linafanya maboresho mengi sana katika huduma zake mbali mbali, mfano Instagram wamekuja na sekunde 60 katika video na Messenger mbioni kuja na ‘Secret Conversation’.
Hii inamaanisha kuwa ‘Secret Conversation’ (Mazungumzo ya siri) yatakuwa yakifanyika katika Messenger baina ya mtu na mtu. Sawa tuna App nyingi sana siku hizi za kutuma na kupokea meseji na kila moja ina faida na hasara zake. Licha ya facebook kuwa moja wapo inaonekana dhahiri kuwa wapinzani wake wanaipa tumbo joto.
![Facebook Messenger](https://teknokona.com/wp-content/uploads/2016/03/1458295721-a64e1dca7612b2af50eb34f56b7a4399-1038x576.jpg)
Facebook licha ya kuwa inajiboresha yenyewe kama yenyewe lakini bado kwa kiasi kikubwa inaangalia wapinzani wake wanafanya nini. Ukifikiria mpango mzima wa ‘Secret Conversations’ wazo moja linaweza likakujia kwamba kipengele hicho kinaweza kikawa kinafanana na kipengele cha SnapChat cha huduma za meseji za kupotea ndani ya muda mchache mara baada tuu ya kusomwa au muda wake kupita (expire).
Pengine labda inaweza ikawa sio meseji za kupotea kama za SnapChat lakini kitu cha kutegemea ni kwamba mazungumzo ambayo yatakuwa yakifanyika ndani ya kipengele cha ‘Secret Conversation’ yanaweza yakawa ya usiri zaidi katika macho ya watu wengine
Mpaka sasa hakuna taarifa kamili kuwa hiyo ‘Secret Conversation’ itakuwa vipi au itakuwa na vitu gani ndani. Cha msingi ni kusubiria taarifa maalumu kutoka kwa Facebook Messenger wenyewe.
![Muonekano Wa Ndani Ya Facebook Messenger](https://teknokona.com/wp-content/uploads/2016/03/Facebook-Messenger-6-840x561.jpg)
Hapa kuna mambo mawili kwani inawezekana ikawa maongezi hayo ya siri yakawa yamefichwa kiasi cha kwamba hata serikali ikashindwa kuyajua au ikawa tuu ni kuyaficha kwa ajili ya macho wa watu wa kawaida tuu – ndio moja kati ya hilo linawezekana au yote kwa ujumla — katika kutumia mtandao wa facebook.
Hii inaweza ikamaanisha kuwa watumiaji wa Messenger wanaweza wakaamua kuficha baadhi ya mazungumzo labda kwa kutumia nenosiri na mazungumzo mengine wakayaacha wazi wazi tuu.
Tusubiria ripoti ya uhakika zaidi kutoka kwao Messenger, lakini kizuri ni kwamba tupo mbioni kupata huduma bora zaidi kutoka kwao kwani wanajali usiri wetu.