Kampuni ya magari ya Volkswagen imejikuta kwenye skendo kubwa sana ambayo hadi kufikia muda huu imesababisha kushuka kwa thamani za hisa zake kwa zaidi ya asilimia 60%. Kampuni hiyo imeshutumiwa na shirika la viwango la Marekani ya kwamba limekuwa likitumia teknolojia kudanganya viwango vya utoaji wa gesi haribifu kwa mazingira kwenye magari yake.
Wadanganya mashirika ya viwango vya ubora wa injini kwa kufanya ionekane baadhi ya magari yake ni bora na mazuri kwa mazingira kuliko hali halisi. Na uongo wote umefanyika kwa kutumia teknolojia tuu.
Elewa udanganyifu huu kwa maneno machache;
Kila injini ya gari huwa inatoa hewa chafu kama sehemu ya utendaji kazi wa injini. Kuna viwango vya ubora wa injini vilivyowekwa na mataifa mbalimbali kwenye nchi zao kuruhusu kiasi cha hewa/gesi chafu inayotolewa na injini za magari.
Kampuni ya Volkswagen imefanya nini hasa?
Kampuni hiyo kutumia chipu za kompyuta zilizopo kwenye baadhi ya magari hayo walifanikiwa kuyawezesha magari hayo kutambua pale ambapo yanaunganishwa na mitambo ya kugundua kiwango cha utoaji wa gesi ya Nitrogen oxide. Yakishatambua ya kwamba yameunganishwa na mitambo hiyo basi yanafanya injini ijiendeshe katika hali ambayo inatoa kiwango kidogo zaidi cha gesi hiyo ukilinganisha na pale ambapo yanakuwa yanatumika barabarani.
Magari ya injini zinazotumia mafuta ya diseli ndiyo yaliyo na teknolojia hiyo ya udanganyifu. Inasemakana magari zaidi ya milioni 11 ndiyo yenye udanganyifu huo na itaitajika zaidi ya shilingi Trilioni 14 kwa ajili ya kuyarudisha magari yaliyonunuliwa kabla na kuyafanyia maboresho.
Hali mbaya ni mbaya kiasi gani?
Kwa nchini Marekani tuu inasemakana ya kwamba kuna magari zaidi ya 480,000 yaliyouzwa kati ya mwaka 2008 na 2015 yaliuzika kupitia vyeti vya usalama wa mazingira vilivyopatikana kwa udanganyifu huo. Yaani ingefahamika mapema basi ‘model’ au aina ya magari ambayo yalipata vibali kuuzika nchini Marekani yasingefanikiwa kufaulu kupata vibali na kama yangepata basi yalitakiwa kupigwa ushuru mkubwa sana.
Tayari mataifa mengine mengi katika nchi zilizoendelea tayari yamesema yataanza kufanya uchunguzi kugundua kama kampuni ya Volkswagen ilifanya udanganyifu huo kwenye nchi zao pia. Kosa hili limeiweka kampuni hiyo katika hali ngumu, watachunguzwa na wanaweza kujikuta katika faini za mabilioni ya pesa. Nchini Marekani wanaweza kujikuta wakipigwa faini ya zaidi ya milioni 70 kwa kila gari lililouzika likiwa na teknolojia hiyo ya udanganyifu. Pia makampuni mengine ya magari yatachunguzwa pia kujua kama utumiaji wa teknolojia hizo za udanganyifu zimetumiwa na wao pia.
Kampuni ya VM imekuwa ni moja ya kampuni inayotengeneza faida kubwa sana na kupata sifa nzuri linapokuja suala la ubora wa teknolojia na hivyo skendo hii inategemewa haitaishia kuharibu mtaji wao katika soko la hisa tuu, skendo hii tayari inaharibu sifa ya muda mrefu ya ubora wa magari yake.
One Comment