Kampuni ya EA Sports, watengenezaji wa magemu maarufu ikiwa ni pamoja na magemu yanayotoka kila mwaka ya mchezo wa mpira wa miguu yanayobeba jina la FIFA wapo katika wakati mgumu baada ya wadukuzi kuweza kuwashinda maujanja.
Toleo jipya la gemu la FIFA 18 lilianza kupatikana rasmi tarehe 29 mwezi wa tisa na ndani ya masaa 24 wadukuzi walifanikiwa kushinda hatua za kiusalama za ndani ya gemu hilo na kuwezesha upatikanaji wa toleo la gemu hilo bure kabisa kwa maelfu ya watu kupitia mfumo wa Torrents.
Baada ya udukuzi huu ina maana mtu yeyote mwenye kompyuta anaweza kushusha/download na kupakua/install toleo la gemu hilo kwenye kompyuta yake bila malipo yeyote.
Nini kilitokea hadi toleo la gemu la FIFA 18 kuweza kuchezewa kiurahisi namna hii kiteknolojia?
Inasemekana kikubwa ni kwamba kampuni hiyo ilibadili teknolojia inayotumia kiulinzi dhidi ya utumiaji wa gemu hilo bila malipo. Kampuni mpya iliyotoa teknolojia ya usalama dhidi ya udanganyifu huo ya Denuvo Technologies imejiweka katika nafasi mbaya kibiashara baada ya tukio hili.
Hii inamaanisha hakuna kampuni nyingine kubwa itaamini kutumia teknolojia ya usalama kutoka Denuvo kwa ajili ya kulinda bidhaa zake dhidi ya udukuzi unaoweza kusababisha kukosekana kwa mapato.
Toleo la FIFA 18 lilikuwa ni moja la toleo la gemu lililokuwa linasubiriwa kwa hamu sana na wacheza magemu ya mpira na inasemekana mapato yake yatakuwa chini ukilinganisha na kama gemu hilo lisingeweza kupatikana kwa njia ya udanganyifu.
Kikundi cha wadukuzi maarufu wa Steampunks ndio kilichohusika na kuwezesha uwezo wa gemu hili maarufu kutumika bure kabisa bila malipo.