Kampuni ya Google imekuwa chini ya uchunguzi wa Tume ya Ushindani ya Umoja wa Ulaya (European Union) kwa muda wa takribani miaka mitano. Mwaka jana ili jambo lilikuwa liishe lakini taarifa zilizotoka ni kwamba Google wana kesi ya kujibu.
Je wamefanya kosa gani?
Kitu kikubwa sana ni kwamba wanashutumiwa na makampuni mengine mbalimbali hii ni pamoja na Microsoft ya kwamba Google wanatumia vibaya ushikiliaji wao wa soko katika maeneo ya Utafutaji Mtandaoni, yaani Google Search na programu endeshaji yao ya Android. Wapinzani wao wanasema Google inatumia huduma hizi kuzipa huduma na bidhaa zake zingine kipaumbele zaidi na hivyo kuzinyama au kuzizuia zile za wapinzani wao kuweza kuonekana na kutambulika kwa watumiaji.
- Google Search
Google wanashikilia soko la utumiaji wa mitandao ya utafutaji barani Ulaya kwa zaidi ya asilimia 90. Yaani zaidi ya asilimia 90 ya watu huwa wanatumia Google katika kutafuta mambo na si kutumia huduma zingine za wapinzani kama vile Bing (inamilikiwa na Microsoft) na Yahoo Search. Kosa linaloangaliwa kwamba Google wanalifanya ni kwamba kupitia Google Search wanaonesha matokeo yanayozidi kuwapeleka watu kwenye huduma zao wenyewe zinazomilikiwa na Google au kutoa matokeo ya ‘Search’ yanayowaletea wao pesa zaidi kupitia matangazo, na katika matokeo haya wanaweka huduma za wapinzani wao kama Microsoft na wengine sehemu ambazo hazionekani kwa haraka kwa watafutaji kama vile wanaowaonesha huduma zinazomilikiwa na Google.
- Google na Android
Google ndio mmiliki mkuu na msimamiaji wa programu endeshaji ya Android na katika makubaliano aliyoyaweka na watengenezaji wakubwa wa simu wanaotumia programu endeshaji hiyo kwenye simu zao kama vile Samsung, HTC, Motorola na wengine wengi ni kwamba ili simu hizo ziendelee kupata masasisho (updates) muhimu kutoka Google ni lazima apps mbalimbali zinazomilikiwa na Google kama vile Google Maps, GMail, YouTube na zingine nyingi ziwekwe kwenye simu hizo kabla hazijamfikia mteja wa simu anayenunua. Suala hili wapinzani wao kibiashara wanasema linawanyima wao kukua kwani ni vigumu sana kwa watumiaji kutafuta apps zingine pale wanaponunua simu ambayo tayari ina apps hizo. Pia linafanya iwe vigumu sana kwa kampuni nyingine inayotengeneza apps kama za Google kuweza kufanikiwa kwani watumiaji hawana sababu ya kutafuta.
Je hii in a maana gani kwa Google?
Ni jambo linalowaumiza kichwa sana kwani kama wakikutwa na hatia ya utumiaji mbovu wa nafasi yao kibiashara kwa kuzuia ukuaji wa makampuni mengine na ubunifu kwa ujumla basi wanaweza kujikuta wakipigwa faini ya mabilioni ya dola za kimarekani na pia wanaweza kujikuta wakilazimishwa kuondoa baadhi ya apps kwenye Android na hivyo kuwapa watumiaji wa simu uhuru wa kuchagua apps za kuweka.
Inasemekana wakikutwa na hatia itawabidi walipe faini ya hadi asilimia 10 ya mapato yao duniani kote kwa mwaka uliopita, mwaka 2014 waliingiza zaidi ya dola bilioni 66 za Kimarekani. (Dola moja = Tsh 1857/=)
Nani mwingine ashawahi kujikuta chini ya panga la Umoja wa Ulaya?
Tume ya Ushindani ya Umoja wa Ulaya tayari ishaadhibu makampuni mengine miaka ya nyuma kwa vitendo vya kibiashara vinavyozuia ukuaji wa biashara na teknolojia.
– Mwaka 2009 Kampuni kubwa ya utengenezaji wa kadi janja (chip) za kompyuta ya Intel ilipigwa faini ya Dola milioni 900 za Kimarekani (Zaidi ya Tsh Trilioni 1.9) kwa utumiaji mbaya wa nafasi yao ya juu sokoni katika eneo lake la kibiashara.
– Mwaka 2004 Microsoft pia walijikuta kwenye wakati mgumu kwa kuambiwa wanatumia vibaya umiliki wao mkubwa wa soko la programu endeshaji ya kompyuta, Windows, kwa kuweka kivinjari chao cha Internet Explorer na hivyo kuzuia ukuaji wa vivinjari vingine kama Opera, Firefox na Chrome. Kesi iyo iliyoanzishwa na malalamiko ya makampuni mengine kuanzia miaka ya nyuma ikaifanya Tume hiyo ya Ushindani kuipiga Microsoft faini ya dola milioni 794 za Kimarekani (Tsh Trilioni 1.4) na pia kuitaka kuondoa kivinjari cha IE na pia programu ya Windows Media Player katika kompyuta mpya zinazouzwa katika Umoja wa Ulaya. Mpaka leo kompyuta za Windows katika bara hilo zinampa mtumiaji chaguo la kuweka kivinjari wanachotaka pale inapokuwa mpya.
“Tunajukumu la kulazimisha makampuni ya kimtandao…..kufuata sheria zetu za Bara la Ulaya” – Afisa wa Tume
Je Google watakutwa na hatia?
Wenyewe Google wanasikitishwa sana mwenendo huu wakidai wanaadhibiwa kwa kuwa wanaongoza/wanafanya vizuri zaidi
Kama umeangalia kosa walilokutwa nalo Microsoft basi ni jambo ambalo halipingiki ya kwamba Google lazima watajikuta katika makali ya panga la Tume hii.
No Comment! Be the first one.