Juzi juzi hivi tuliandika kuhusu Google kuwa chini ya uchunguzi wa kibiashara unaofanywa na Tume ya Ushindani wa Kibiashara ya Umoja wa Ulaya kuhusu Android..Tume hii inajiandaa kuipata faini Google wiki hii itakayovunja rekodi kuhusiana na huduma yake ya Search.
Faini kubwa zaidi inayoshikilia rekodi kwa sasa kuwahi kutolewa na tume hiyo ni Euro bilioni 1.06 ambayo ilitolewa kwa kampuni ya chips ya Intel mwaka 2009. Intel walikuwa na hatia ya kulipa baadhi ya watengenezaji kompyuta ili wasitumia chips za mshindani wao wa biashara, kampuni ya AMD.
Euro bilioni 3 ni takribani Tsh Trilioni 7.45 / Ksh Bilioni 342.
Faini hii ya Euro bilioni 3 inahusisha uchunguzi uliofanywa na tume hiyo kati ya mwaka 2010 hadi 2012 kuhusu huduma ya ‘Search’ (utafutaji) ya Google. Google walishitakiwa ya kwamba wanatumia huduma yao ya Google Search kutangaza zaidi huduma zao za mauzo (shopping) huku wakifanya matoleo ya huduma za makampuni mengine kuwa chini zaidi.
Wenyewe Google wamejitetea wakisema huduma yao ya Search haiathiri wapinzani wao kwa kuwa kwa sasa kuna huduma nyingi za kimauzo zinazofanya vizuri tuu – mfano Amazon, Ebay n.k.
Google wapo katika wakati mgumu sana kama faini hii itadondoshwa kama ilivyo kwani tayari pia wanasuburia matokeo ya uchunguzi wa jinsi wanavyoendesha biashara yao ya programu endeshaji ya Android – unaweza soma kuhusu hili hapa -> Google kuchunguzwa na chombo cha biashara cha Umoja wa Ulaya.
Nani mwingine ashawahi kujikuta chini ya panga la Umoja wa Ulaya?
Tume ya Ushindani ya Umoja wa Ulaya tayari ishaadhibu makampuni mengine miaka ya nyuma kwa vitendo vya kibiashara vinavyozuia ukuaji wa biashara na teknolojia.
– Mwaka 2009 Kampuni kubwa ya utengenezaji wa kadi janja (chip) za kompyuta ya Intel ilipigwa faini ya Dola milioni 900 za Kimarekani (Zaidi ya Tsh Trilioni 1.9) kwa utumiaji mbaya wa nafasi yao ya juu sokoni katika eneo lake la kibiashara.
– Mwaka 2004 Microsoft pia walijikuta kwenye wakati mgumu kwa kuambiwa wanatumia vibaya umiliki wao mkubwa wa soko la programu endeshaji ya kompyuta, Windows, kwa kuweka kivinjari chao cha Internet Explorer na hivyo kuzuia ukuaji wa vivinjari vingine kama Opera, Firefox na Chrome. Kesi iyo iliyoanzishwa na malalamiko ya makampuni mengine kuanzia miaka ya nyuma ikaifanya Tume hiyo ya Ushindani kuipiga Microsoft faini ya dola milioni 794 za Kimarekani (Tsh Trilioni 1.4) na pia kuitaka kuondoa kivinjari cha IE na pia programu ya Windows Media Player katika kompyuta mpya zinazouzwa katika Umoja wa Ulaya. Mpaka leo kompyuta za Windows katika bara hilo zinampa mtumiaji chaguo la kuweka kivinjari wanachotaka pale inapokuwa mpya.
Tutaendelea kufuatilia maendeleo ya chunguzi hizi na kukupa habari zaidi. Je kwa mtazamo wako unaona ni sawa kuibana sana Google wakati bado watu wanaweza tumia huduma nyingine nyingi zaidi katika masuala ya ununuaji bidhaa (shopping) kama vile mitandao ya Amazon, eBay n.k?
Chanzo: The Inquirer na mitandao mbalimbali