Eric Schmidt, mwenyekiti wa Google ametamka kwamba kampuni yake itarejea Uchina siku za karibuni.
Kampuni ya Google ilijitoa nchini China mnamo mwaka 2010 baada ya kampuni hiyo kutokubaliana na sera za kuficha/kutoruhusu baadhi ya tovuti na huduma kuoneshwa nchini China (“censoring”), huku walilalamika kwamba serikali ya nchi hiyo ilikuwa inahusika katika udukuzi uliolengwa kwao na makampuni mengine machache.
Bw. Schmidt alisikika akitoa maneno hayo yanayoendana na maneno ya muanzilishi mwenzake wa Google, Sergey Brin, wakati wa maonesho ya kiteknolojia huko mjini Beijing. Sergey Brin yeye amesikika akisema ya kwamba kuna baadhi ya huduma za Google zitarudishwa kwenye Jamhuri ya Watu wa Uchina.
Kwa mujibu wa Eric Schmidt, Google haikujitoa Uchina moja-kwa-moja bali kuna harakati walibakisha na uamuzi huo umewapa muda wa kutengeneza mahusiano na baadhi ya makampuni ya nchini humo ambayo yameonesha nia ya kufanya biashara na Google.
Soko la Uchina lina changamoto lukuki ila linavutia biashara nyingi kutokana na fursa inayotokana na wingi wa wachina wenye kipato cha juu. Kampuni kama Apple zinaendelea kujizatiti na kuvuna fursa hii kwa hiyo siyo haba nao Google wakajipanga tena kurudi kwenye soko hilo.
Mabadiliko katika muundo wa makampuni ya Google ya zamani ndani ya muunganiko mpya wa Alphabet unaweza ukazipa uhuru baadhi ya huduma za Google kuanza kufanya kazi mapema zaidi ya nyingine ndani ya Uchina-bara. Wachambuzi wengi wanategemea kwamba Google Playstore mahsusi kwa ajili ya nchi ya Uchina itakuwa huduma ya kwanza kutolewa tena.
One Comment