Kuna uwezekano Google wapo mbioni kutengeneza simu ya kwao ambayo itaendeshwa na mfumo wa Android ili kuweza kupambana na iPhone. Mpango huu ukikamilika Google watakuwa wameingia katika ushindani na makampuni yanayotengeneza simu janja.
Kwa nini Google waje na simu zao?
Google wamekuwa wakibuni simu zinazokwenda na jina la Google Nexus lakini wamekuwa wakishirikiana na watengenezaji wa simu kama vile Samsung, Huawei, Motorola na LG katika utengenezaji simu hizo.
Ingawa kwa kiasi fulani hii ilisaidia kuongeza ushawishi wa Android lakini haikufanikiwa kusaidia katika mpambano dhidi ya Apple na pengine jambo hili ndio limepelekea kwa kampuni hii kuamua kuingia katika utengenezaji wa simu hizo kabisa.
Google wanataka kuweza kusimamia kila sehemu ya simu hizo, kuanzia ubunifu na sifa zake za ndani na ata masasisho yatakayokuwa yanatolewa na ujio wa matoleo mapya ya Android. Haya ni mambo ambayo yanazipa sifa kubwa simu za iPhone kutoka Apple.
Kwa sasa masasisho (updates/upgrades) hazijawa zinatolewa kwa haraka na watengenezaji simu kama vile Samsung na wengine jambo ambalo limekuwa likiigharimu Android katika ushindani na iOS.
Tetesi hizi za kampuni hii kuleta simu ya kwake sio mara ya kwanza kusambaaa mtandaoni ingawa mara kadhaa maafisa wakubwa wa kampuni hii wamekuwa wakikataa kuthibitisha tetesi hizi.
Kwa mujibu wa mtandao wa The Telegraph Google wapo katika mazungumzo na mitandao ya simu mikubwa kwa ajiri ya kukamilisha taratibu za mpango huo, simu hiyo itatengenezwa na kuingia sokoni mwishoni mwa mwaka huu na hii ni kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika pia.
