‘Kwenye nia siku zote pana njia’. Usemi huu unadhihirika baada ya ile bajaj yenye kutumia nishati ya Jua kuwasili nchini Uingereza baada ya kukwama nchini Ufarasa kwa zaidi ya wiki moja.
Takribani wiki moja hivi TeknoKona ilikuhabarisha kuhusiana na bajaji iliyokwama safari yake kutokana na dereva wa bajaji hiyo kuibiwa nyaraka yake ya kusafiria (passport), hatimaye dereva bajaji hiyo amefanikiwa kufika Uingereza.
Safari hiyo ilidumu kwa miezi saba na umbali ukiwa maili 6,200 (9,978 Km). Alitarajia kufika mapema lakini akakwama kwa muda Paris baada ya pasipoti na kipochi chake kuibiwa.
Mmiliki wa bajaj hiyo alisema kuwa watu hupenda bajaji yake na hujitokeza na kupiga selfie. Watu hushangaa sana anapowaambia kuwa bajaji yake haitumii mafuta.
Alianzia safari yake Bangalore nchini India kisha akaendea Iran. Alipitia Uturuki, Bulgaria, Serbia, Austria,Uswizi, Ujerumani na Ufaransa. Anapanga kuhitimisha safari yake katika kasri la Buckingham, London.
Ni safari iliyokuwa na changamoto kadhaa lakini hatimaye lengo la kuhamaisha watu kutumia magari yanayotumia kawi mbadala kama vile solar au umeme limetimia.
Vyanzo: BBC, mitandao mbalimbali