Kwa sasa kila mtengenezaji wa simu anajaribu namna ya kuweza kutengeneza betri itakayoweza kudumu kwa muda mrefu zaidi, hii itawawezesha watumiaji wa simu janja kuweza kufurahia zaidi simu zao bila kuogopa kuhusu chaji zao.
Watengenezaji wa simu za Huawei katika kuhangaikia swala hili wamekuja na ubunifu mpya wa betri ambayo itachukua muda mdogo zaidi kuichaji, hii itasaidia watumiaji kuwa na uwezo wa kuchaji simu zao mpaka zijae bila ya kusubiri muda mrefu.
Huawei wameonesha katika video jinsi battery iliyoisha chaji ikiwekwa katika kifaa cha kuchajia na kisha kwa dakika 5 betri hiyo inaoneshwa ikiwa imejaa kwa 48%, hii ni mara kumi zaidi ya muda unaotumiwa na battery ya kawaida(yenye ukubwa sawa) kufikia kiasi hicho cha chaji.
Battery hii imefanyiwa mabadiliko makubwa katika uundwaji wake ili kuipatia huu uwezo mkubwa wa kuchaji kwa haraka, ubunifu huu hata hivyo hautaathiri uwezo na maisha ya betri kwa baadaye bali betri itabaki na uwezo wake uleule.
Ingawa hii teknolojia bado haijafikia kiwango cha uzalishaji kwa watumiaji wa kawaida ila tutegemee mabadiliko makubwa pindi hatua za uzalishaji zitakapofikiwa, vifaa kama simu janja, saa janja na tableti vitauchukua mfumo huu na hivyo mifumo yake kwa ujumla itabadilika.
Tusubiri tuone jinsi teknolojia nzima ya simu itakavyobadilishwa na ugunduzi huu maana betri imekuwa ndio kikwazo kikubwa kwa mambo mengi kufanikiwa katika sekta hii. Teknolojia nyingi kwenye simu janja zimekua kwa kasi lakini katika eneo la betri bado kasi yake ni ndogo.
One Comment