Kampuni ya Tecno inasifa moja kubwa nayo ni kufanikiwa kutengeneza simu zenye viwango vizuri pale ukilinganisha na bei za simu husika, na katika simu ya Camon C8 bado Tecno wanaendelea kuhakikisha sifa hiyo inaendelea kuwepo.
Nimeitumia simu ya Camon C8 kwa siku kadhaa na ninachoweza sema hii ni simu nzuri na yenye ubora wa kuvutia, kama wewe ni mpenzi wa kupiga picha basi utaipenda ata zaidi.
Kwenye Tecno Camon C8 msisitizo umewekwa zaidi katika eneo la ubora katika upigaji picha.
Tazama uchambuzi kwa njia ya video kupitia akaunti yetu ya YouTube
Muonekano
Kwa kiwango cha ukubwa mfano basi unaweza linganisha Tecno Camon C8 na ukubwa wa simu za Samsung Note na ata iPhone 6S Plus, ina kioo (display) kikubwa cha inchi 5.5 kilicho na ubora wa HD – High Definition.
Kamera
Kama nilivyogusia mwanzoni ya kwamba kama wewe ni mpenzi wa upigaji picha basi Tecno Camon C8 haitakuangusha – inakuja na kamera ya nyuma yenye MegaPixel 13 wakati ya mbele kwa ajili ya selfi inakuja na MegaPixel 5. Ukilinganisha, iPhone 6S Plus kutoka Apple inakuja na kamera ya MegaPixel 12 kwa nyuma huku ya mbele zikiwa sawa kwa MegaPixel 5.
Pia kamera yake ya nyuma ina flash mbili ili kuhakikisha unapata picha nzuri ata ukiwa gizani, ina uwezo wa ‘Autofocus’ unaokuwezesha kupata picha za muonekano mzuri zaidi.
Diski Ujazo
Tecno Camon C8 inakuja na diski ujazo wa GB 16, kama utaona ukubwa huu haukutoshi basi utaweza kutumia memori kadi (SD Card) na ina uwezo wa kupokea hadi memori kadi ya ukubwa wa GB 32.
Programu Endeshaji
Android 5.0 Lollipop – inakuja na toleo zuri tu la programu endeshaji ya Android. Simu nyingi za Tecno zinatumia toleo la Android 4 na hivyo Tecno Camon C8 imekuwa moja ya simu mpya kabisa katika utumiaji wa toleo la Android Lollipop.
Vipi kuhusu prosesa, RAM na mengineyo?
Inakuja na prosesa ya ‘quad-core’ yenye kiwango cha 1.2 GHz hii ikiwa na pamoja na RAM ya GB 1. RAM GB 1 ni kiwango kinachotosha tuu katika kuhakikisha simu yako inaweza kufanya kazi vizuri ata pale ambapo kuna apps kadhaa zinafanya kazi kwa wakati mmoja.
Inakuja na betri lenye kiwango kizuri tuu cha chaji, nacho ni mAh 3000, kwa kiwango hichi basi utegemee si chini ya siku nzima ya bila kuchaji katika matumizi ya kawaida.
Pia simu hii ya laini mbili. Unatumia laini ya kawaida, na ndogo (Micro SIM Card).
Pia inakuja na microUSB, teknolojia ya Bluetooth, pamoja na WiFi.
Tecno Camon C8 inapatikana kwa takribani Tsh 350,000/=, kutegemea na eneo uliopo basi bei inaweza ikawa chini au juu kidogo ya hapo.
One Comment