Baada ya uvumi ya kwamba wameachana kabisa na biashara ya utengenezaji simu kampuni ya Sony imetoa simu mpya yenye sifa za kuvutia. Simu hiyo inayoendelea kutumia jina maarufu la Xperia, imetambulishwa kama Sony Xperia Z4.
Kwa muda mrefu watu walikuwa wameelewa Sony watakuwa washakata tamaa kabisa na biashara ya simu baada ya kupata hasara sana kwa kipindi kirefu katika biashara hii. Utoaji huu wa simu mpya na yenye kiwango cha juu unaonesha bado Sony hawajakata tamaa kuweza kupata mafanikio katika biashara hii.
Sony wameitambulisha simu hiyo rasmi nchini Japan na itaanza kuuzika katika nchi hiyo kabla ya kusambaa kwa nchi zingine duniani kote. Ingawa simu hiyo inakuja na jina la Xperia kampuni ya Sony imefanya mabadiliko kadhaa kuifanya Xperia hii kuonekana tofauti zaidi.
Je ina nini kikubwa?
Kwanza inakuja na kava (body) la mchanganyiko na chuma na kioo, kizungu ‘mental-and-glass body’. Hili inaifanya kuwa na hadhi kubwa kiubunifu kulinganisha na simu janja nyingi zinazokuja na maplastiki.
Kioo?
Inakioo chenye ubora wa hali ya juu kimuonekano, kioo chake cha inchi 5.2 kina kiwango cha 1080p hivyo tegemea kuangalia video za kiwango hadi cha HD katika ubora unaovutia.
Kamera?
Ni nomaaaa, simu hii inakuja na kamera yenye ubora wa MegaPixels 20.7, hichi ni kiwango kikubwa sana kulinganisha na simu janja nyingi za bei ya juu ambazo mara nyingi kiwango kinakuwa chini ya MegaPixels 18. Na kwenye kamera kwa ajili ya selfi ina kiwango cha juu cha MegaPixels 5.
Kulinganisha: Samsung Galaxy S6: Kamera ya nyuma – MegaPixels 16, ya selfi – MegaPixels 5
Betri?
Betri linakiwango cha 2930mAh, hichi ni kiwango kizuri sana kulinganisha na uwezo mkubwa wa simu hii, kulinganisha kwa haraka fahamu simu mpya kutoka Samsung ya Galaxy S6 inakuja na betri ya 2550mAh.
Wenyewe Sony wanadai ya kwamba kwa kiwango hichi cha betri mtumiaji ataweza kutumia Z4 kwa zaidi ya masaa 17 ya maongezi simu ikiwa kwenye 3G kabla ya kuchaji tena. Hii inamaanisha katika hali ya kawaida tegemea kuchaji mara chache zaidi ukilinganisha na simu janja nyingi zilizo sokoni kwa sasa.
Prosesa?
Inakiwango kizuri cha prosesa kinachoweza kuifanya simu hii kuweza kuhimili apps zinazoitaji kiwango kikubwa cha prosesa. Inakuja na Snapdragon 810 yenye ubora wa 2GHz 8-core 64bit.
RAM?
Kwenye simu mbalimbali ambazo nishawahi kuzifanyia uchambuzi humu ndani nimekuwa nikiongelea suala la ubora wa prosesa wa kutegemea kwenye simu janja ya uhakika. Mara nyingi nimesema kama pesa unayo basi hakikisha simu janja unayonunua ina angalau si chini ya GB 1 kwenye RAM, kwenye hili Sony wameamua kufanya kweli. Xperia Z4 inakuja na RAM kiasi cha GB 3.
Programu Endeshaji?
Ni Android, na kwa uzuri zaidi ni Android 5.0, yaani toleo la kisasa zaidi la Android Lolipop.
Mengineyo?
- Simu hii haitaweza kuingiza maji na uchafu kwa urahisi, yaani ni ‘water-and-dust-resistant’.
- Itakuja kwenye rangi 4 hii ikiwa ni pamoja na nyeupe, nyeusi, ya shaba na ‘aqua green’
- Inauzito wa gramu 144
- Inakuja na diski uhifadhi (Storage) wa GB 32, lakini pia utaweza kutumia memori kadi
- Teknolojia zingine za kimawasiliano kama Bluetooth, WiFi n.k
Bei?
Bado bei rasmi ya simu hii haijatolewa ila inategemewa kufahamika ndani ya siku chache zijazo.
No Comment! Be the first one.