Kuna mambo mengi ya kuzingatia wakati ununuzi wa Kompyuta mpya. Lakini wengi wetu tunapotaka kununua Kompyuta yapo tunayoyazingatia. Zaidi huwa tunaangalia ukubwa wa RAM,
Hard disk, CPU, GPU na kadhalika.
Lakini linapokuja sula la kuchagua kati ya 32-Bit au 64-Bit, hapa huwa hatujali sana vyovyote itakavyokuwa kwetu ni sawa tu. Aidha iwe na Prosesa yenye 32-Bit au 64-Bit.
Wengi hatuzingatii hapo kwa kuwa hatujui nini maana ya kuwa na 32-Bit au 64-Bit. lakini wengine wamekuwa na swali la kujiuliza nini tofauti ya 32-bit na 64-Bit.

Kwa watumiaji wa Windows wanaponunua programu au game mara nyingi huona chaguo kati ya
32-Bit au 64-Bit.
Lakini ni nini tofauti kati ya 32-Bit au 64-Bit?
Mfano rahisi sana ambao kila mmoja anaweza kuuelewa ni kwamba 32-Bit au 64-Bit, ni sawa na barabara yenye njia mbili(32-Bit) na nyingine ina njia nne(64-Bit).
Kwa kawaida barabara yenye njia nne itapitisha magari haraka kuliko yenye njia mbili. Tofauti yake ni hiyo japo ufanyaji kazi wake wa kila kitu utakuwa sawa.
Tofauti nyingine ya kutumia Kompyuta yenye 64-Bit inaonekana wazi pale unapohitaji kuweka RAM kubwa zaidi. Kwa kawaida mfumo wa 64-bit unaweza kuweka RAM zaidi ya 4GB na kuendelea kuliko 32-Bit ambao mwisho wa kiwango cha utumiaji wa RAM ni 4GB.
Pamoja na tofauti hiyo Kompyuta yenye Prosesa ya 64-Bit inaweza kutumia mfumo endeshi wenye 64-Bit au 32-bit. Hata hivyo mfumo endeshi wa 32-Bit kwenye Prosesa ya 64-Bit utafanya kazi lakini si kwa
uwezo wake kamili – haishauriwi.
Kama matumizi yako ni ya kawaida tu katika Kompyuta yaani hufanyi kazi nzito kama Video Editing na 3D graphics, wala huchezi game hutagundua tofauti yoyote kati ya 32-Bit na 64-Bit.
Kwa hiyo ni dhahiri kuwa processor 64-bit ina uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kuliko 32-bit.
Ushauri unapotaka kuweka Windows yoyote katika Kompyuta yako ni vizuri kujua Prosesa yake ni ipi kati ya 32-Bit au 64-Bit. Kwani Windows nayo huja na aina mbili za matoleo yake ima la 32-Bit au 64-bit. Lakini habari nzuri ni kwamba laptop nyingi sana za kisasa siku hizi zinatengenezwa katika uwezo wa 64-bit hivyo unaweza kuweka toleo la Windows lolote kulingana na utumiaji wako.
Pengine baada ya maelezo hayo ungependa kujua Kompyuta yako ni 32-Bit au 64-Bit. Ili kujua hilo nenda katika Run kisha andika msinfo32 halafu bonyeza ok utakuja ukurasa ambao utakuonesha maelezo yote kuhusiana na Kompyuta yako.
- Angalia palipoandikwa System type. Utaona pameandikwa X86-based PC au X64-based PC.
- Cha kuzingatia ukiona system type ina X86 fahamu hiyo 32 bit prosesa
- Na ukiona system type ni X64 basi fahamu hiyo 64-Bit prosesa.