Miezi ya karibuni, makampuni ya Samsung, Apple na Google yote yalifanya mikutano mikubwa ya kutamba na teknolojia mpya, sambamba na kutambulisha simu zao za hali ya juu – Samsung S5 na Note 4, Apple i-phone 6 na 6-Plus na Google Nexus 6, ambazo zinakusanya kila aina ya ujuzi ambao makampuni hayo yamejitutumua kupata ili kuendeleza teknolojia ya mawasiliano ya kisasa.
Kikubwa kinachozungumziwa mpaka muda huu ni ukubwa wa simu zao ila kuna mambo machache ya muhimu ya kuzilinganisha na kuzitofautsha kimatumizi zaidi, ikiwemo ubora wa kamera, skrini kwa ajili ya burudani na jinsi zinavyosaidia kukamilisha kazi kwa ufanisi, vitu ambavyo vinaboresha maisha yetu ya kawaida.
Kwa Burudani:

Katika sekta ya rubudani (Kama rafiki zetu wa kimasai wanavyosema), tunaangalia zaidi ubora wa skrini, uwezo wa sauti na ukubwa na nguvu ya prosesa.
Samsung wanatamba na skrini zenye mng’ao wa teknolojia ya Quad HD Super AMOLED Display, skrini ambazo zina uwezo wa kupambanua rangi nyingi zaidi katika mwanga tofauti na ukubwa wa inchi 5.7 kwa Note 4 na inchi 5.1 kwa S5. Skrini za I-phone za Apple zina ukubwa wa inchi 4.7 na 5.5, ambazo ni chini kidogo ya Samsung ila nazo zinatamba kwa mng’ao wa Retina HD Display ambao unasifiwa zaidi na mashabiki wa Apple kuwa wa ajabu kupindukia, ukiwa na uwezo wa kuonyesha rangi halisi zaidi. Kama ukubwa wa skrini ni kigezo chako cha uchaguzi, Google Nexus hapa inaweza kuwa mshindi, kwani inafunika simu zote ikiwa na inchi 6 za nguvu na mng’ao wa Quad HD Display.
Katika hili suala la skrini, simu zote hapa zinaweza kupata maoni tofauti kutoka mashabiki wake ila ukweli ni kwamba skrini zote zina mng’ao wa kushangaza, pengine kupitiliza mahitaji ya kwaida ya kibinadamu ya kuangalia muvi na kucheza magemu,
Kwa upande wa sauti, Google Nexus 6 inasifiwa sana kwa ubora wa sauti kuliko simu nyingine kwani ina spika mbili zinazotoa sauti ya ‘stereo’ kuelekea mbele, huku ripoti nyingine zikisema kuwa sauti kwenye spika ya i-phone ni ya kawaida ingawa ina spika mbili zinazoelekeza sauti chini ya simu, huku Samsung, zikiwa na spika moja nyuma ya simu hutoa sauti ya isiyo ya kushangaza pia.

Simu zote zina prosesa bora zaidi iwezekanavyo, kwahiyo kucheza magemu kwenye simu hizi ni jambo rahisi sana.
Kwa Maisha na Ndugu, Jamaa na Marafiki:
Kamera imekuwa kitu cha muhimu sana katika simu ya kisasa. Uwezo wa kamera hizi umekuwa ukiimarika sana, kiasi kwamba tutaendelea kushuhudia zikiondoa umuhimu wa kubeba kamera za kawaida na mwaka huu Samsung, Apple na Google wanatamba kwa namna tofauti jinsi walivyoweza kuboresha uchukuaji wa picha na simu zao za hali ya juu.
Samsung wanategemea ukubwa wa megapixeli 16 kwenye kamera yao ya nyuma ya Note 4 huku Apple i-phone na megapixeli 8, wanategemea teknolojia yao ya iSight na facetime kunogesha picha za i-phone 6 bila ya wewe kuhangaika sana. Kwa upande wa tatu, Nexus wao wamejikita zaidi kwenye kumpamtumiaji urahusi wa kupiga picha za hali ya juu bila ujuzi mwingi na hivyo wametoa vikolombwezo vingi kwenye appu ya kamera.
Vikolombwezo hivyo hatahivyo vinaweza kupatikana ukiingia kwenye kumbukumbu za picha (‘Gallery’) kama utataka kurekebisha picha zako. Kwenye upande wa picha zenye uhai, yani video, i-phone 6 wamehamisha teknolojia yao ya picha kwenye video pia kwahiyo, video utakazochukua kwenye kamera ya i-phone itaongezewa manjonjo na simu yenyewe moja kwa moja.
Samsung wao wanatamba kwamba utafurahia mipangilio mbalimbali ya video-kamera ikiwemo mpangilio utakaokuwezesha kuchukua video za kasi zaidi ya zote na unaweza hata pia kamua kuachana na video na badala yake ukachukua picha ya kawaida ikiambatana na sauti.
Kwenye Nexus, Google wanatamba kwamba watu wanapenda urahisi zaidi, kwa hiyo ukifungua camera ya Nexus hautakutana na manjonjo mengi zaidi ya batani kadhaa za kuchukua picha na video zenye mng’ao zaidi ya HDR+.
Kwa Kazi:

Katika suala zima la kufanya kazi, unaweza kusema kwamba Samsung wako mbele zaidi na pengine siyo sawa kuzilinganisha iphone 6 na Nexus na Note 4, labda S5.
Sifa kuu ya Note 4 ni uwezo wa kutumia S-Pen kwa kunakili. Safari hii, S-Pen ya Note 4 imeongezewa ubora zaidi ya Note zilizopita. Samsung wenyewe wanasema kwamba wamefanya unakili wa S-Pen kuwa karibu sana na kuandika kwa peni ya kawaida kwenye karatasi.
Unaweza kunakili hadi kwenye picha utakazochukua pamoja na kunyakua chochote kwenye skrini ya simu yako na kukiweka kwenye nyaraka zako, kufanya urahisi wa kufanya mambo ya kiofisi muda wowote, hata ukiwa kwenye mkutano.
Pia, Samsung wanatamba na teknolojia yao ya kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja kwa kugawanya skrini ya Note. I-phone wao ingawa hawana mbwembwe nyingi kama hizi za Note 4, wanakupa uhakika kwamba utatumia simu yako kwa muda mwingi zaidi, hadi masaa 12 bila ya kuchaji tena na prosesa yao ya A8 ya bit 64 yenye nguvu ya kufanya kazi zako kwa haraka zaidi, mambo ambayo ni ya msingi kwa kufanya kazi nyingi kwenye simu.
Nexus wao wanategemea prosesa yao ya Qualcomm® Snapdragon™ 805 processor ya bit 64 kukusaidia kukamilisha kazi zako kwa haraka na wakitamba zaidi kwa uwepo wa appu nyingi zaidi kwenye soko lao la Androidi kufanya kazi yoyote!
Hitimisho
Kuchagua simu ya hali ya juu hasa kama kujizawadia au kumpa zawadi mtu kipindi hiki cha siku kuu, inategemea sana na mazoea ya mtu mwenyewe na ushabiki wake kwa mfumo flani au kmpuni flani. Simu za i-phone, S5 na Note 4 pamoja na Nexus 6 zote ni za hali ya juu na teknolojia zake ni jambo la kustaajabisha na tofauti sana na simu ya hali ya chini.
Hakuna kinachotenganisha sana simu hizi hata kwa bei. Labda kitu kitakachobadili mawazo yako ni utofauti wa i-phone na hadhi yake- ni kitu tofauti sana na simu hiyo itakupa hadhi tofauti sana na mtu wa kawaida. Kwa upande mwingine, kwa nchi zetu za Afrika, ukinunua Samsung, umenunua zaidi ya simu – utakuwa umenunua na ‘customer care’ inayokujali sana, kwa mfano, masaa machache baada ya kununua simu yako ya Samsung ya hali ya juu na kuisajili vyema, utapigiwa simu na kuulizwa kama unafurahia au la ili hatua sahihi za kukuridhisha zichukuliwe. Hautapata ‘kupetipeti’ kama huku kwa kampuni nyingine zaidi. Kwa upande wa tatu, Ukichagua Nexus, unachagua Android iliyo ‘bikra’, yani android ambayo haijaguswa na kujazwa mambo usiyotaka zaidi ya kitu kinachotoka moja kwa moja kutoka wazazi wa Android – Google na hivyo utategemea ‘droid’ isiyo na kasoro hata kidogo. Mwisho wa siku, chagua linabaki kuwa lako, umezoea au unapendelea kampuni gani zaidi?
No Comment! Be the first one.