Muonekano wa kawaida wa tovuti ya Familia ya Kifalme ya Uingereza umebadilika baada ya kutangazwa kwa kifo cha Malkia Elizabeth II. Kwa sasa umewekwa ukurasa wa muda katika tovuti hiyo wenye rangi nyeusi na picha ya Malkia Elizabeth II katika siku ya kuapishwa kwake mwaka 1953.
Tovuti hiyo pia inaonyesha tangazo fupi kutoka kwa Jumba la Buckingham kutangaza kifo cha mtawala huyo mwenye umri wa miaka 96. Ukurasa huo unaonyesha mwaka wa kuzaliwa kwa Malkia na mwaka wa kifo – 1926 hadi 2022. Sehemu ya chini ya ukurasa huo ina ujumbe unaosema: “Tovuti rasmi ya Familia ya Kifalme haitapatikana kwa muda wakati mabadiliko stahiki yanafanyika.”

Taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa huo inasomeka: “Malkia alikufa kwa amani huko Balmoral mchana huu. “Mfalme na Malkia Consort watasalia Balmoral jioni hii na watarejea London kesho.”
Jambo hili siyo jipya kufanyika katika tovuti hiyo, Baada ya kifo cha Philip Duke wa Edinburgh mwaka 2021, ukurasa wa muda uliwekwa wakati kumbukumbu zake zikipakiwa na kitabu cha maombolezo cha mtandaoni kikiundwa.

Kwa kawaida tovuti hii huwa na habari kuhusu Familia ya Kifalme ya Uingereza, Misaada na Ufadhili wa Malkia na Diary ya Kifalme pamoja na taarifa zingine kuhusu utawala wa kifalme.
Pamoja na hayo akaunti zote za mitandao ya kijamii za Familia ya Kifalme ya Uingereza zimebadilishwa muonekano baada ya kutangazwa kwa kifo cha Malkia Elizabeth II.

Mabadiliko mengine yanayotarajiwa kufanyika katika tovuti hiyo ni pamoja na Tangazo la kuapishwa kwa Mfalme wa Uingereza Charles III.
No Comment! Be the first one.