Hivi karibuni unaweza jikuta umenunua kompyuta mpyaaaa alafu ikatae kuwekwa Windows 7 na 8.1. Yaani zaidi ya kutumia toleo la Windows 10 haitakubali Windows 7 au 8 au ata itakapokubali haitafanya kazi kwa ufanisi mzuri.
Katika uamuzi ambao umewashangaza wengi kampuni ya Microsoft imesema itanyima kutoa huduma ya maboresho (updates) kwa baadhi ya kompyuta mpya zitakazokuwa zinatumia prosesa za kisasa zaidi pale ambapo programu endeshaji nyingine nje ya Windows 10 ikitumika.
Uamuzi huu unaonekana kama moja ya hatua ambazo Microsoft wanazifanya ili kuzidisha utumiaji wa Windows 10, ishafahamika ya kwamba kuna watumiaji wengi ambao bado wanaona bora wabakie kwenye Windows 7 na 8.1.
Uamuzi huu utawafanya watu ambao wanataka kuwa na kompyuta za kisasa zaidi wawe wanafahamu ya kwamba lazima itawabidi watumie toleo la Windows 10 kwenye kompyuta hizo.
Prosesa za kisasa zinazokuja kutoka makampuni makubwa ya utengenezaji wa prosesa tayari kupitia ushirikiano wa makampuni hayo na Microsoft tayari aina ya prosesa kadhaa zimeshawekwa kwenye kundi la prosesa spesheli zitakazoweza fanya kazi na Windows 10 tuu na si toleo la nyuma zaidi ya hapo. Prosesa hizo ni pamoja na Kaby Lake kutoka kampuni ya Intel, 8996 kutoka kampuni ya Qualcomm pamoja na prosesa za jamii ya Bristol Ridge kutoka kampuni ya AMD.
Uamuzi huu utaathiri zaidi kompyuta / laptop mpya sana ila kwa kompyuta nyingi zinazopatikana madukani kwa sasa tayari zinaweza fanya kazi na Windows 7 na 8.1 na kupata masasisho (updates) kutoka Microsoft bila shida yeyote.
Matoleo ya programu endeshaji ya Windows 7 na 8.1 yataendelea kupata updates (masasisho) bila shida kadhaa kwa miaka kadhaa. Windows 7 itaendelea kupata masasisho ya usalama hadi Januari 14 mwaka 2020, wakati toleo la Windows 8.1 litaendelea kupata masasisho hadi Januari 10 mwaka 2023. Ila utapata masasisho (updates) kama tuu unatumia matoleo hayo katika kompyuta zenye sifa ya kutumia matoleo hayo.
Kwa mtazamo wa wengi uamuzi huu unaonekana ni wa kuzidi kujihakikishia toleo la Windows 10 linazidi kutumika na utumiaji wa matoleo yaliyopita ukipungua.
Je kwa mtazamo wako unafikiri ni maamuzi mazuri?
vyanzo: The Forbes, The Verge
No Comment! Be the first one.