Watu wengi hawajui ni jinsi gani mitandao kama vile kupatana na Inauzwa.com inavyojiingizia pesa. Wengi wanafikiria inatoa huduma zake bure tuu, nafikiri cha muhimu kujua hapa ni kwamba hakuna cha bure duniani.
Mitandao hii mara nyingi inakuwa inasaidia watu katika kuuza vitu ambavyo hawavitumii tena kwa urahisi. Kwa mfano unaweza ukauza gari, nyumba au hata simu yako ya zamani baada ya kupata mpya kupitia mitandao hii.
Kwa Tanzania mtandao wa aina hii ambao unasikika sana ni kupatana.com lakini je, unajua ni jinsi gani mtandao huo unavyotengeneza mkwanja?
NJIA
1. Kupitia Google AdSense
Hii ni njia maarufu sana ya kutengeneza pesa kupitia mtandao. Kama unaweza kupata watu wengi wanaotembelea mtandao wako mara kwa mara, basi unaweza kuweka matangazo kutoka Google na kuanza kupokea pesa.
Hapa ishu nzima iko hivi, kuna makampuni au watu ambao huwa wanailipa Google ili iwatangazie bidhaa zao. Google inatafuta sehemu za kutangaza bidhaa hizi kulingana na mwenye bidhaa anataka itangazwe wapi na kwa nani. Mitando kama kupatana yenyewe inajiunga na huduma ya kupokea matangazo kutoka Google.
Baada ya kujiunga Google inawapa matangazo, hapo mtu akiingia katika tangazo hilo kampuni litalipwa. Malipo yatatokana na makubaliana baina ya kampuni na Google na namba ya watu walioliona tangazo hilo
2. Kupitia Kwa Wauzaji Wa Bidhaa Zao Kupitia Mtandao Huo
Katika mitandao kama vile Kupatana.com mtu ukitaka kutangaza kitu na upate mteja kwa haraka inabidi ilipie tangazo lako. Yaani inabidi uwalipe kupatana ili waweze kulionyesha tangazo lako mara nyingi zaidi kwa watu wengi zaidi.

Hii inamaanisha yale matangazo mengine ambayo watu wametuma katika mtandao huo hayatapata kipaumbele kama tangazo lako ambalo umelilipia. Watu wengi huwa wanalipia matangazo yao kama wakiwa wanauza vitu vya thamani kubwa kama vile magari, nyumba, madini n.k au wanapotaka kupata mteja wa bidhaa zao haraka iwezekanavyo.
3. Kupitia Matangazo Ya Kawaida
Kupitia mitandao ya kupatana.com au mitandao mingine ya kawaida, mitandao hiyo inaweza ikajipatia pesa kwa kuweka matangazo ya kawaida tuu. Kwa mfano unaweza ingia katika mtandao ukakutana na tangazo la kampuni la Voda, Tigo n.k. Hapa inamaanisha kuwa makampuni haya yanalipa mitandao kama Kupatana.com katika kuonyesha matangazo yao katika mitandao hiyo
Kwa haraka haraka ni kwamba mitandao hii inapata pesa kutoka Google, Kwetu sisi (wauzaji wa bidhaa zetu kupitia mtandao huo) na hata kwa makampuni mengine. Ni sawa mitandao hii kwa macho ya kawaida unaweza ukasema kwamba inatoa huduma ya bure katika jamii kwani watu wengi hujiunga katika mitandao hiyo na kuuza vitu vyao bure. lakini kama nilivyosema hapo awali, hakuna cha bure…