WhatsApp imekuwa maarufu kweli na kila kukicha maboresho yanaongezwa na kuifanya kuzidi kuvutia na kuwa na watumiaji wengi zaidi.
Kama moja ya njia rahisi ya kufanya mawasiliano basi si ajabu kuwa na vitu vidogo vidogo ambavyo ni wajanja wachache ndio wanavifahamu na pengine ulikuwa hufahamu kuwa unaweza kuficha mazungumzo kwenye WhatsApp kwa sababu mbalimbali.
Kwanini mtu anaamua kuficha (kuweka sehemu moja) mazungumzo kwenye WhatsApp?
Zipo sababu kadha wa kadha lakini binafsi nitaongelea mbili ambazo naziona zina uzito wa kipekee ndani yake:
Kuwa na mazungumzo na watu wengi ambayo hutaki kuyapoteza. Hii inadhihirika pale ambapo ukifungua WhatsApp kwenye uwanja wa wale wote ambao umefanya nao mazungumzo wanafikia watu 30 au na zaidi, hapa inaweza kuwa ngumu kumpata mtu ambaae uliwasiliana nae siku/wiki kadhaa zilizopita.
Kutotaka mtu mwingine afahamu kuwa una mawasiliano na mtu fulani. Kama simu janja yako inashikwa na wengi na wewe si mtu wa kutumia neno siri kwenye simu lakini kuna mazungumzo ambayo hupendi mtu mwingine aone, hii inaweza kuchukua uwamuzi wa kuficha mazungumzo hayo ili kulinda heshima, maelewano, n.k kwa yule/wale wanaopenda kuperuzi kwenye simu yako.
Jinsi ya kuficha mazungumzo kwenye aina mbalimbali za WhatsApp.
Mpaka hivi leo naamini kabisa utakuwa unafahamu kuwa kuna aina tofauti tofauti za WhatsApp mbali na ile ambayo inapatikana kiurahisi kwenye App Store/Play Store; FMWhatsApp, WhatsApp Beta, GBWhatsApp, n.k.
Kama unatumia WhatsApp/WhatsApp Beta kwenye simu yako bofya kwa sekunde kadhaa (mpaka alama ya pata itokee) mazungumzo yote ambayo unataka kuyaficha kisha ubofye kitufe cha pili pembezoni juu upande wa kulia (kitufe cha pili kutoka kulia baada ya zile nukta tatu) na hapo utakuwa umefanikiwa kuficha.

Jinsi ya kuona/kufichua mazungumzo kwenye WhatApp.
Sijawahi kushangaa mtu akiniambia “Nimebonyeza sehemu fulani kwenye WhatsApp na sasa hivi mazungumzo yetu siyaoni”. Kwa teknolojia ya simu za mguso hicho kitu kinawatokea watu wengi tu. Sasa ukitaka kuona yale mazungumzo yote uliyoyaficha kwenye WhatsApp, wewe shuka mpka mwisho wa wale watu wote uliowasiliana nao na utaona neno hili “Archived” bofya hapo na utayapata mazungumzo yote ambayo hupendi yaonekane kirahisi.

Unaweza ukutaka kuondoa mazungumzo yako na mtu fulani kutoka kwenye “Maficho”, hapa unaingia kwenye maunguzo ambayo umeyaficha (archived) kisha unabofya kwa sekunde kadhaa (mpaka alama ya pata itokee) mazungumzo yote ambayo unataka kuyaficha kisha ubofye kitufe cha pili pembezoni upande wa kulia juu (cha pili baada ya zile nukta tatu) na hapo utakuwa umefanikiwa kumuondoa mhusika kutoka ulipokuwa umeficha.

Jinsi unavyoweza kuficha/kufichua mazungumzo kwenye GBWhatsApp.
GBWhatsApp ina mambo mengi kweli lakini kwenye kipengelecha kuficha au kuona mazungumzo ambayo yameficha nawapa alama za za juu aliyeandika programu hii (GBWhatsApp). Ukitaka kuficha mazungumzo unashikilia kwa sekunde kadhaa kisha unabofya kwenye zile nukta 3 upande wa kulia juu kisha utachagua neno hide.

Pale unapotaka kuona kile ambacho umekificha utabonyeza neno WhatsApp halafu kuna menyu itatotekea na basi utachora ile alama uliyoiweka kwa ajili ya ulinzi na mazungumzo yote ambayo umeyaficha utayaona.

Kuficha ama kutoficha kuna faida na hasara zake lakini mwamuzi ni wewe mwenyewe utakavyoona inakupendeza na kwa sababu teknolojia imeletwa itusaidie basi tuitumie vyema.
Vyanzo: Tovuti mbalimbali