Neno Siri (Password) imara ni kazi sana kutengeneza, kukumbuka na hata kuliandika. Pengine ndio sababu watu wengi hupendelea kutengeneza neno siri dhaifu (rahisi) ili kuepusha shida za kusahau n.k.
Watu wanapenda miteremko sana na hiyo inawapelekea watengeneze neno siri rahisi sana kuliko inavyobidi. Lakini kumbuka neno siri hilo linaweza kukusaidia kwa mengi mfano kuwaweka mbali wapekuzi wa mitandaoni na akaunti zako za mtandaoni.
Hongera kwako! TeknoKona inajua mbinu kadhaa za kufanya neno siri lako kuwa imara. Lakini kabla hatujaenda moja kwa moja kujua namna ya kufanya hivyo, ngoja kwanza tujikumbushe vitu vitatu muhimu vinavyo hitajika wakati wa kutengeneza neno siri.
1. Usifanye Neno Siri Kuwa Rahisi Kuotea
Usipendelee kutumia neno siri ambalo mtu anaweza otea kwa urahisi kwa mfano “123456,” “123456789,” “password,”, maneno haya ni rahisi kuotea. Pia epuka kutumia jina lako, la ndugu au hata mtu wa karibu kama neno siri. Pengine wewe unaweza ukaona umetengeneza neno siri gumu lakini kwa mtazamo mwingine ikiwa sio kama unavyofikiria.
2. Tengeneza Neno Siri Lenye Herufi 8 Na Kuendelea
Hapa saa nyingine ndio watu wanapo ona ni mzigo. Je nitaikumbuka? ndio maswali watu wanayojiuliza sana. Kwa nini nisiweke “12345678” tuu, maana ndio itakuwa rahisi kukumbuka?. Vyanzo vinasema Neno siri lenye herufi chache ni rahisi sana kugunduliwa na wataalamu wa ku ‘hack’ tofauti na neno refu. lakini pia cha kuweka akilini ni kwamba neno refu hilo pia linabidi lisiwe rahisi kuotea kwa mfano ‘123456789’ neno kama hilo sawa ni la herufi nane na kuendelea lakini bado lina dosari.
3. Usitumie Neno Siri Moja Kila Sehemu
Kama unatumia neno siri lako hilo hilo katika sehemu nyingi tofauti tofauti pia likitokea la kutokea ni rahisi sana data zako kuvuja au kuibwa kwa urahisi. Pata picha Mitandao ya kijamii yote unatumia neno siri moja. Kama hiyo haitoshi pata picha unatumia neno siri moja katika akaunti zako zote za benki. Ni hatari sio?
Tujifunze Jinsi Ya Kuwa Na Password (Neno Siri) Imara Sasa!
Kwa haraka haraka tuu, Sheria za kutengeneza neno siri imara ni kama zifuatazo.
- Inabidi iwe na herufi za aina mbali mbali yaani kubwa na ndogo upande wowote (mwanzo. katikati au mwishoni)
- Inabidi iwe na herufi 8 na kendelea
- Tumia neno siri linalojitegemea kwa kila akaunti
Ni hayo tuu, Lakini Neno siri Kama “KonA0611YTT” Ni imara sana, na sio rahisi kulikumbuka, au sio? Ngoja nikuonyeshe nimelitengeneza vipi.
Kwanza anza kufikiria sentensi mbali mbali bila mpangilio, unaweza ukatumia usemi au hati meneno katika nyimbo. Mfano mimi nimechagua neno siri (“KonA0611YTT”) katika mtandao namba moja tanzania katika maswala ya teknolojia yaaani TeknoKona – Kona Ya Teknolojia Tanzania. Kutoka hapo Nimechukua neno Kona katikati nikaweka tarehe na siku ya kuzaliwa kwangu mwishoni nikamalizia na YTT (Ya Teknolojia Tanzania). Hiyo Yote inatengeneza neno “KonA0611YTT” ambalo limekidhi mahitaji yote ya neno siri. Maneno siri mengine kwa muonekano sio rahisi kuyashika lakini kutukana na upatikanaji wake inafanya yawe rahisi sana.
MUHIMU: Neno “KonA0611YTT” sio neno siri kwa kitu/mtu/akaunti chochote/yeyote katika mtandao wa TeknoKonaDotCom
2 Comments