Simu mpya za iPhone, 6s/6s Plus zina uwezo wa kurekodi video katika kiwango kikubwa cha ubora, yaani 4K.
Japokuwa si matoleo ya mwisho ya uwezo wa kamera kutoka kampuni za Apple, lakini video zinazorekodiwa na kamera hizi ni nzuri ajabu, hata kupita uwezo wa baadhi ya kamera za kawaida zinazotumika kila siku.
Ndio maana, kituo cha televisheni kutoka Switzeland, Leman Bleu kimeaamua kutumia simu za iPhone kama mbadala wa kamera zao za kawaida katika kurekodi matukio yote ya kila siku yanayorushwa na kituo hicho.
Kila mwandishi wao wa habari amekabidhiwa iPhone 6 pamoja na ‘Selfie Stick’ wakitakiwa kutumia simu hizo kurusha matukio ya moja kwa moja au kurekodi kwa kutumia simu hizo.
Mwongozaji wa vipindi vya TV Laurent Keller amefafanua kuwa, kutumia iPhone hakurahisishi tu ubebaji, bali pia unapunguza gharama kubwa. Kwa kutumia iPhone, waandishi sasa wanaweza wakafanya kazi kubwa zaidi bila kuhofia mzigo wa kamera kubwa za kuandalia kazi zao.
Baada ya kutangaza ujio wa iPhone 6 mwaka jana, Apple walikuja na kampeni iliyoitwa ‘Shoot with iPhone 6’, ili kuonyesha umaridadi wa kamera zao, na sasa kampeni hiyo inaendelea kupata umaarufu maradufu.
Japokuwa uwezo wa iPhone wa kurekodi picha hauko chini ya uwezo wa kamera za kawaida, lakini waandishi wa kituo icho watatakiwa kujifunza mbinu mpya za kurekodi kutumia iPhone.
Mwaka jana, kituo kimoja cha Charlotte, N.C. kiliwahi kujaribu kuandaa kipindi kwa kutumia vifaa vya Apple, lakini kutokana na kutokuwa na mbinu za namna ya kupiga picha kwa kutumia vifaa hivyo, walisitisha baada ya kupata picha ambazo hazikuwa na ubora wa kuweza kurushwa katika televisheni.
Sasa mfumo huu unatazamiwa kuungwa mkono na makampuni mengi zaidi ya utangazaji, hasa baada ya kutangazwa kwa simu mpya za iPhone 6s/6s Plus zenye uwezo wa megapixeli 12, ‘image stabilization’ na video za 4K. Kwa hivi, teknolojia ya utangazaji inatazamiwa kuwa rahisi kuliko kawaida.
iPhone wanaendelea kuwa magwiji wa tasnia ya upigaji picha, kwa kuleta teknolojia ajabu ya sensa za kamera, kuwawezesha wapiga picha na wachukua video kupiga picha zinazovutia Zaidi, zinazoweza kuchapishwa kwa ubora zaidi, na kwa gharama nafuu Zaidi ikilinganishwa na kamera za kawaida.
Kama hukujua, idadi kubwa zaidi ya matangazo duniani kwa sasa yanarekodiwa kwa kutumia vifaa vya IOS. Na kukushangaza zaidi, filamu maarufu ya Tangerine kutoka Hollywood ilizua mjadala mkubwa baada ya kubainika kuwa filamu nzima ilirekodiwa kwa kutumia iPhone 5s mbili (2) pekee.
Chanzo cha Makala haya ni mtandao wa iMore na Cultofmac.
One Comment