Kwa kiasi kikubwa mashambulizi makubwa ya programu endeshaji yaliyohusisha ransomware (mshambuliaji kuteka mafaili/data za kompyuta) yamekuwa yakitokea kwa programu endeshaji ya Windows zaidi na si kwa OS X.
Lakini sasa inasemekana kuna waliofanikiwa kutengeneza shambulizi la kwanza la aina hiyo lililofanikiwa kuwafikia baadhi ya watumiaji wa programu endeshaji ya OS X.
Ransomware (Programu za Utekaji) ni kitu gani?
Hizi ni programu ambazo kama zikiingia kwenye kompyuta yako basi zitasoma data yako na kuchagua kukuzuia kufungua mafaili flani hadi pale utakapotuma pesa kwenda akaunti zao na wao kukupatia nywila (password) ya kuyapata mafaili hayo yaliyotekwa kwenye kompyuta yako mwenyewe.
Kwa miaka kadhaa mara nyingi hili limetokea kwa watumiaji wa programu endeshaji za Windows zaidi. Na ilionekana ni kitu kigumu kusambaa kwenye programu endeshaji wa OS X inayotumika kwenye kompyuta za Apple.
Shambulizi limefikaje kwa watumiaji wa OS X?
Utafiti umeonesha ya kwamba kirusi kinachosambaza programu hiyo kimepitia watu walioshusha programu ya kudownload mafaili katika teknolojia ya Torrent iitwayo Transmission.
Uchunguzi wa toleo la programu ya Transmission lililokuwa linapatikana kupitia mtandao wao kwa siku ya Ijumaa unaonesha code ya Ransomware ilikuwa ndani yake na wote walio’install’ toleo hilo basi waliingiza kirusi cha Ransomware katika kompyuta zao.
Programu ya Transmission ni programu ya bure, ya muda mrefu na yenye sifa ya usalama. Inaonekana wadukuzi wa mtandao (hackers) waliingia kwenye mtandao huo na kuweka toleo la programu hiyo ambalo waliliboresha likiwa na programu yao ya ransomware.
Mtandao wa Transmission ushasafisha na kuondoa faili hilo na kurudisha yaliyosafi. Walioathirika na shambulizi hilo wanasema walitakiwa kutoa dola 400 za kimarekani (Takribani Tsh 800,000=) ili waweze ku’unlock’ mafaili yao yaliyofichwa kwenye kompyuta zao.
Malipo hufanyika kupitia malipo ya njia ya siri ya BitCoin ambayo huusisha namba spesheli bila kuonesha/kupatikana kwa taarifa zozote kati ya mtumaji na mpokeaji.
Habari nzuri ni kwamba imeonekana ili kufanikisha shambulio la Ransomware (programu utekaji) katika kompyuta zinazotumia OS X ni juhudi ndefu sana kama ukilinganisha na jinsi ya kufanikisha shambulio kama hilo katika kompyuta za Windows – ransomware inaweza pitishwa ata kwa kufungua faili la PDF lililowekwa programu hiyo.
Mwezi uliopita hospitali moja jijini Los Angeles ililazimika kulipa takribani Tsh 37,200,000/= | Kes 1,723,800/= ili kuweza kutoa lock iliyokuwa imewekwa kwenye mafaili ya rekodi za wagonjwa pale kompyuta zake ziliposhambuliwa na programu ya Ransomware (wanatumia Windows).