Umenunua simu mpya na sasa unataka kuachana na ile ya zamani, iwe kwa kuuza au njia yeyote ile…ni hatua gani za kuhakikisha umezifuata data muhimu na binafsi?
Leo tutakueleza hatua muhimu za kufuata ili kuhakikisha data zako zinakuwa salama. Usije muuzia mtu simu leo halafu kesho akawa na data zako zote muhimu.

Hatua ya kwanza kabisa, bila kujali simu unayotumia
- Fanya backup ya data zako zote muhimu, hii ikiwa ni pamoja na namba za simu. Kama unatumia android unaweza fanya backup za namba za simu na picha kwa kutumia huduma ya Google na nyingine nyingi. Kama ni iPhone unaweza tumia iCloud au kwenye kompyuta kupitia iTunes.
- Hakikisha unatoka (logout) kwenye akaunti za mitandao ya kijamii
- Kama simu ina memori kadi unayolenga kuihamisha pia basi kumbuka kuitoa, na kama utaiuza pamoja na simu basi kumbuka kuifuta kabisa pia (format).
- Weka rekodi ya namba ya kiwandani (serial number) ya simu yako, hii ni muhimu kwani chochote kikitokea mbeleni uwe na rekodi ya bidhaa uliyoiuza.
Hatua hizi zingine ndio za kuhakikisha usalama zaidi wa data kwako pale unapouza simu; iwe ya Android, au iOS.
Mambo ya Kufanya Kabla ya Kuuza au Kubadilisha Simu: Unapouza simu ya Android
Njia salama na bora zaidi kufanya kitu kinaitwa ‘factory reset’. Kuzidi kuhakikisha data zako ziko salama kumbuka kwenda kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook na kufuta kabisa simu hiyo.
Pia unaweza kwenda mtandao wa Google eneo la akaunti na kufuta kabisa simu hiyo kutoka kwenye akaunti yako. Google – www.myaccount.google.com , kisha nenda ‘Sign-in & Security’, kisha ‘Device activity & notifications’, tafuta simu husika na kisha sehemu ya Account Access bofya ‘Remove’.
Mambo ya Kufanya Kabla ya Kuuza au Kubadilisha Simu: Kwa iPhone iOS
Kwa mtumiaji wa simu ya iPhone, toleo la iOS 5 kuendelea ni salama zaidi kwa njia za ufutaji data. Programu endeshaji, iOS, inahakikisha ni vigumu sana mtu yeyote kupata data zako kama ukifuata hatua hizi kwa usahihi kabisa.
- Nenda Settings>iCloud>Find My iPhone, ingia na zima uwezo wa utafutaji simu (Zima)
- Pia ‘logout’ akaunti yako ya iCloud, kufanya hivyo nenda Settings>iCloud na kisha nenda kwenye ‘Sign Out’, kama unatumia iOS 7 au zaidi basi bofya ‘Delete Account’ yaani futa akaunti.
Ni muhimu kufanya ‘sign out’ kwani kama ukifuta vitu vyako bila kujitoa kwenye akaunti ya iCloud hii ina maanisha ya kwamba vitu hivyo vitafutwa pia kwenye akaunti ya iCloud. Hivyo ni muhimu ulogout kwanza akaunti ya iCloud kabla ya kuanza kufuta data zako.
- Hatua ya tatu na muhimu ni kulogout akaunti ya Apple ID, hii ni pamoja na iMessage.
Kulogout iMessage nenda Settings>Messages
Kulogout iCloud nenda Settings>iTunes & App Store – kisha bofya barua pepe yako na kisha chagua ‘Sign Out’
- Hatua inayofuata ni kufuta kabisa data zako, kufanikisha hili nenda Settings> General> Reset> Erase All Content and Settings, kubali na utakuwa umefuta data zote kwenye simu yako rasmi.