Je ushawahi kusikia kuhusu taasisi ya ShuleDirect na ukawa bado una maswali kuhusu taasisi hiyo? Leo fahamu zaidi.
TeknoKona tumejitahidi na tukafanikiwa kumpata dada Faraja Nyalandu, muanzilishi (founder) wa ShuleDirect na kumuuliza maswali machache yanayoweza kukufahamisha yote muhimu kuhusu taasisi ya ShuleDirect na juhudi/harakati zao katika eneo la elimu.
1. Kwa mtu ambaye leo ndio mara ya kwanza kusikia kuhusu ShuleDirect ungeweza kumwambia ni kitu gani kwa ufupi?
Shule Direct ni taasisi inayotumia mifumo ya kiteknolojia kama mtandao na simu za mkononi kuwawezesha wanafunzi na walimu kupata elimu bora.
2. Wazo la ShuleDirect lilikujaje? Ni matatizo gani hasa yanatatuliwa kwa uwepo wa ShuleDirect?
Wazo lilianza baada ya matokeo mabaya ya mitihani ya Taifa ya kidato cha Nne yaliyotoka mwaka 2013. Kipindi hicho Mwanzilishi wa Shule Direct akiwa amemaliza masomo yake ya Digrii ya Sheria nchini Uingereza alikuwa amerejea nchini tayari kwa kazi katika taaluma aliyosomea. Mojawapo ya vitu vilivyomwezesha kusoma na kufaulu vizuri Digrii yake ni kuweza kusoma kutumia mitandao mbalimbali akiwa katika uzazi na ulezi wa watoto wake wawili aliojaaliwa kuwapata akiwa masomoni. Teknolojia ilimuwezesha kuwa mama na kuwa mwanafunzi kikamilifu.
Tatizo kubwa linalotatuliwa na Shule Direct ni ukosefu wa rasilimali bora za elimu za kujifunza kwa upande wa wanafunzi na za kufundishia kwa upande wa walimu.
3. Kwa sasa huduma ya ShuleDirect inaweza patikana kupitia njia zipi? – Je kuna mpango wa kuongeza njia nyingine zaidi?
Unaweza kupata rasilimali za kujifunza, kufanya mazoezi, kujipima na kujadiliana za masomo tisa ya Sekondari na elimu nyingine zisizo rasmi lakini muhimu kwa maendeleo ya vijana kwenye mtandao wa www.shuledirect.co.tz.
Sehemu ya pili inayokupa nyenzo zote hizo na huduma ya kumuuliza maswali mwalimu wetu ‘genius’ Ticha Kidevu, ni kupitia MAKINI SMS ambapo inapatikana kupitia ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu za mkononi za aina zote (sio lazima iwe smartphone) kwa kutuma neno MAKINI kwenda 15397 kwa watumiaji wa Tigo.
Na sehemu ya tatu na ya mwisho kwa sasa ni mfumo wa kompyuta wa kujifunza maalumu kwa ajili ya shule zenye vyumba vya kompyuta na majumbani kwa kiingereza unajulikana kama Learning Management System ambao unafanya kazi bila kutumia mtandao (internet) au data. Ukiwa na mfumo huo unaweza kupata rasilimali zote za tovuti yetu ya www.shuledirect.co.tz moja kwa moja bila gharama ya intaneti.
4. Tokea kuanza kwenu hadi sasa, je changamoto kuu 3 mnazokutana nazo ni zipi? Na je mmejipanga vipi dhidi ya changamoto hizo
Changamoto kubwa ni teknolojia. Katika teknolojia kuna gharama za kutumia teknolojia iwe data au manunuzi ya kifaa cha kutumia, kuna suala la uhakika wa upatikanaji wake kwasababu sio kila sehemu mitandao inafika na cha tatu ni ufahamu wa watumiaji wa Teknolojia.
Ukiona mtiririko wa jinsi tulivyotengeneza huduma zetu utagundua kila kilichomfuata mwenzako ilitokana na tulichokiona kwenye jamii kama changamoto na hivyo kutumia hiyo kama fursa ya kutengeneza huduma inayotatua au kupunguza makali ya changamoto hiyo.
Hatubuni kitu bila maoni na tafiti za watumiaji wa huduma zetu na jamii kwa ujumla. Kwa mfano tuligundua zaidi ya 80% ya watumiaji wetu wa mtandao wa www.shuledirect.co.tz walikuwa wanatumia opera mini browser. Hii idadi ilikuwa inaakisi takwimu za Taifa zinaoonyesha watumiaji wa smartphones ni chini ya asilimia 20. Tulikuwa na mpango wa kutengeneza app kwa kipindi hicho lakini azma yetu ni kuwezesha wanafunzi kupata elimu bora tena wale ambao kikawaida hawana mbadala na kama upo basi una gharama kubwa ambayo hawaimudu. Tukaona ni bora tuwafikie katika mfumo wa mawasiliano ambao tayari wanautumia tena kwa zaidi ya asilimia 80, hivyo tukaanzisha MAKINI SMS.
4. Haraka haraka, Je wewe unaiona ShuleDirect itakuwa wapi ndani ya miaka 2 – 3?
Naiona Shule Direct ikifikia wanafunzi zaidi ya milioni moja Tanzania lakini naiona ikivuka mipaka na kwenda nchi nyingine za Afrika kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kupata elimu bora.
5. Gharama – Je ni kwa asilimia ngapi huduma zenu ni za bure? Na zile za kulipia mnadhani bei mliyoiweka itaweza kuwa ya kawaida (sio ghali) kwa wengi?
Ndoto yetu ni kuona wanafunzi wengi wanapata elimu bora na kufanikiwa katika masomo yao na hatimaye kufanikiwa maishani. Hivyo basi, tunaamini hii ni huduma kwa jamii na hatuwezi kuitumia kupata faida, kwahiyo asilimia 75% ya huduma zetu ni bure na kidogo kinachotozwa kwa mtumiaji ni kutuwezesha kuendelea kutengeneza rasilimali nyingi na kubuni teknolojia nyingine bila kutegemea sana wafadhili.
5. Una neno gani kwa wanafunzi ambao bado hawajajaribu kutumia huduma za ShuleDirect?
Elimu ni haki yako. Elimu ni kama daraja la kukufikisha kwenye ndoto zako. Sisi tunaamini kuwa kwakuwa ni haki yako, basi inabidi uipate mahali popote na muda wowote. Na sio elimu tu, bali elimu bora, karibuni sana Shule Direct.