Apple kuja kukuruhusu kutengeneza iPhone yako mwenyewe iwapo imeharibika. Uwezo huo umetangazwa na Apple ambapo wamesema wataanza kuuza vipuri mbalimbali kama vile betri, kioo (display) na kamera za iPhone na baadae kuanza kuuza hadi vipuri vya kompyuta za Macbook.
Kwa muda mrefu Apple imekuwa ikiendesha huduma za utengenezaji simu kupitia makubaliano na biashara chache tuu, wao pekee ndio walikuwa wanauwezo wa kununua vipuri vya ubora sahihi na pia walikuwa wakipata mafunzo kutoka kwa Apple. Hii imechangia kufanya gharama za utengenezaji wa vifaa vya Apple kuwa juu sana.

Baada ya kesi kadhaa katika mahakama mbalimbali nchini Marekani pamoja na mapendekezo ya kisheria kutoka kwa vyama vya watumiaji kwenye majimbo kadhaa nchini Marekani pamoja na bara la Ulaya, inaonekana Apple amekubali kuwapa haki wateja ya kufanya matengenezo wenyewe.
Right to Repair – Harakati za watu kupigania haki ya kupewa uwezo wa kufanya matengenezo ya vifaa vyao imekua kwa kasi. Rais Biden wa Marekani ni mmoja wa watu wanaokubali haki hii, na amesema serikali itafanya jitihada za kisheria kuhakikisha uhuru huu unapatikana kwa wateja.
Apple wamesema wanaleta duka la mtandaoni la vipuri muhimu, duka hilo litaweza kutumiwa na mtu yeyote kwa kuanzia huduma itaanza kupatikana Marekani kabla ya kusambaa kwenye mataifa mengine.
- Mtu ataweza kupata kitabu cha muongozo wa jinsi ya kufungua, na kubadilisha kipuri cha aina ya kifaa chake.
- Ataweza kufanya manunuzi ya vifaa vinavyosaidia kufungua na kufanga kifaa chake mf. simu, kwa usalama.
- Pia ataweza kununua kipuri chochote anachohitaji, kwa kuanzia vipuri vya iPhone 13, 12 na SE vitaanza kupatikana.

Kwa simu za Android tayari makampuni kama HTC, Samsung, Google na ata Microsoft kupitia vifaa vya Windows wameshawawezesha wateja wao kufanya hivyo. Makampuni haya yanashirikiana na tovuti na huduma ya iFixit kuwapatia watumiaji miongozo ya utengenezaji pamoja na uwezo wa kununua vipuri orijino kwa ajili ya vifaa vyao.
Duka hilo la mtandaoni litaanza kupatikana hivi karibuni kupitia tovuti ya Apple, na kwa kuanzia litaanza kuhudumia Marekani kabla ya kuanza kupatikana kwenye masoko mengine muhimu.
Je wewe ni mtundu wa kujitengenezea vifaa vyako vya elektroniki? Basi hii itakuwa ni habari njema, ila kama wewe sio mtundu sana bado unashauriwa kutumia huduma spesheli za matengenezo kuepuka kuharibu zaidi kifaa chako kwa kutokujua baada ya kukifungua.
Chanzo: Apple
No Comment! Be the first one.