Kama hutaki mwizi au ukipoteza simu yako mtu aweze kupekenyua vitu vyako, unahitaji kuwekea kifaa chako loki ambayo italinda hasa hasa zile data zako za muhimu.
Loki zipo za aina nyingi sana siku hizi –Asante kwa kukuwa kwa teknolojia – kuna zile za kutumia kidole, ‘pattern’ na hata zile za kuweka namba na maneno kama kawaida.
Kwa mfano watumiaji wengi wa simu za android wamezoea ‘pattern’ (ile loki ya kuunganisha vile vidoti doti). Sasa ni makosa gani yanafanyika katika kuweka loki vifaa vyetu?
Hapa tunafeli sehemu moja, wengi wanaotaka kuweka loki katika vifaa vyao wanapenda kuweka loki rahisi ambayo wataweza hata wao kuikumbuka mara moja tuu. Lakini kumbuka sio vizuri kuweka loki rahisi kwani ni rahisi sana watu kuotea loki hiyo.
Kwa mfano nenosiri kama “0000,” “1111,” “1234” au “0852 (kucheza na vibonyezo vya kati),” sio za kuzitegemea kabisa kwani ni rahisi sana mtu kuziotea.
Lakini unaweza sema kuwa sababu watu hawapendi kuwa na nenosiri refu sana ni kwamba linatesa kila mara kuliandika wakati unatumia simu yako. Fikiria kwa siku unaangalia simu yako mara ngapi? Sasa pata picha kila mda huo unakuwa unaandika nenosiri ambalo ni refu sana.
Nadhani kutokana na jambo hili ndio maana watengenezaji wa simu janja na tablet wameamua kuja na njia rahisi kabisa kama vile kwa kutumia sense za vidole, kwa kutumia uso na ‘Pattern’ (maarufu katika simu za Android).
Kwa watu wengi kuchora Pattern ni njia wanayoipenda zaidi kwani ni rahisi sana kuiingiza na pia ni rahisi kwa vichwa vyetu kuikumbuka mara moja. Pia kwa sababu kuna pointi 9 inazobidi uziunganishe hivyo inafanya kuwe na aina nyingi ambazo mtumiaji anaweza seti neno siri lake.
TATIZO KUHUSU PATTERN
Katika auchunguzi uliofanywa na aliyekuwa mwanafunzi wa chuo cha Norwegian University of Science and Technology, Marte Løge, alibaini kuwa kati ya ‘pattern’ 4000 asilimia 77 walikuwa wanaanza kuchora kuanzia katika moja kati ya kona nne za juu kabisa. Asilimia 40 walianza katika kona ya juu upande wa kushoto kabisa.
Kwa haraka haraka watu wengi huwa wanaanza kuchora ‘pattern’ zao na kwa kupitia katika vinundu vine tuu mpaka vitano saa zingine. Kwa kufanya hivyo wanashusha ule ugumu wa kuweza kutoa loki hizo. Sawa kwa mtu kukisia bado ni vigumu lakini kwa watu ambao wamebobea katika kazi hizo, wadukukuzi (hackers) wanaweza wakawa wamerahisishiwa kazi kwa kiasi flani.
Katika ‘Pattern’ kuweka shepu za herufi kama vile “L” au “Z” kuanzia katika kona ya kushoto ya juu ni rahisi sana kwa mtu kuotea kwani zinajulikana sana. Pia watu wanafeli pale wanapoweka refu hizo kutoka kwa majina yao au kutoka kwa watu wao wa karibu.
Nadhani kama tunakubaliana kuwa kama unatumia aina hizo za ‘Pattern’ ni rahisi sana mtu kuiotea na akafanikiwa kutoa loki katika kifaa chako. Sasa ni njia gani za kufanya kuhakikisha kuwa unakuwa na ‘Pattern’ ambayo sio rahisi kwa mtu kuiotea?.
TENGENEZA PATTERN NGUMU
Kitu cha kwanza kabisa cha kufanya ni kwamba tengeneza ‘pattern’ ambayo itahusisha vile vinundu 8 au 9. Mdukuzi au hata mtu anaekupekua ni vigumu sana kuotea ile yenye vinundu 8 mpaka 9 kwa sababu mara nyingi watu wanatumia vinne mpaka vitano.
Hata kwa kutumia vinundu vingi, kumbuka usitumie vinundu hivyo katika kutengeneza ‘pattern’ yenye umbo la herufi kwani itakua nib ado rahisi kuikisia. Cha kufanya hapa anza kuchora ‘pattern’ hiyo kwa kuanzia vinundu vya kati
Kwa mfano angalia hii (lakini usitumie hii kama ilivyo)
Itakuwa ni vigumu kwa mtu kuweza kuiotea hii sio? Hata saa nyingine mtu akikuona kabisa unaiandika hii bado inaweza ikawa ni vigumu kwa yeye kuikumbuka.
ONGEZA ULINZI ZAIDI
Kwa kawaida ukiwa unachora pattern yako kuna kimstari kinaonyesha ulipoanzia kuchora mpaka unapoishia. Hii ni sawa tuu na kuonyesha neno siri lako tuu wakati unaliandika (show password). Ni nzuri kwa kukusaidia kuepuka kukosea wakati wa kuchora lakini kumbuka watu walio karibu na wewe na wao wanaweza wakaona
Cha kufanya katika kifaa chako chako cha Android nenda katika Settings>>Security and uncheck “Make pattern visible.” Ili kubadilisha. Katika vifaa vingine unaweza ukakuta katika Settings>>Lock Screen. Hapa sasa kwa mtu ambae ana nia ya kukuangalia atashangaa tuu vidole vinapita haraka katika vinundu kwa haraka na bila shaka atashindwa kukariri.
2 Comments
Comments are closed.