Kampuni ya vifaa vya elekroniki ya Logitech imeinunua kampuni ya Jaybird ambayo ni kampuni inayotengeneza vifaa vya teknolojia ya wireless, hii inaonekana ni jitihada za kampuni ya Logitech kutawala soko la vifaa vya muziki vya wireless.
Logitech imelipa dola za kimarekani milioni 50 taslimu kwaajiri ya ununuzi huo huku ikiwa imetoa ahadi ya kuongeza mpaka dola milioni 45 iwapo kampuni hiyo mpya itaweza kufikia malengo ndani ya miaka miwili ijayo.
Jaybird ni kampuni ambayo inayojulikana na kuheshimika katika soko la vifaa vya muziki vya wireless, hivyo ununuzi huu unaifanya Logitech kuwa na nguvu zaidi katika utengenezaji wa vifaa vya muziki vya wireless ambavyo vinategemewa kuhitajika katika soko kwa wingi baada ya makampuni ya simu kuacha kutengeneza earphone zinazotumia jack ya 3.5mm ambayo imekuwa ikitumika kwa miaka mingi sasa.
Earphone zenye jack ya 3.5mm huenda zikapotea baada ya watengenezaji wasimu kutaka kuiondoa ili kupunguza ukubwa wa simu na nafasi yake kuchukuliwa na vitu vingine kama spika za kawaida. Apple ni moja ya watengenezaji wa simu ambao tetesi zinasema kwamba wataachana na earphones hizo za zamani, kampuni hii imeona fursa hii na inataka kuwa ndiyo watengenezaji wa earphones za wireless ambazo zitakuwa zinahitajika baada ya 3.5mm kuachwa.
Logitech wanasema kwamba pamoja na kuinunua kampuni hiyo ya Jaybird itaendelea kutumia jina hilo hilo la kibiashara, huku Jaybird itanufaika kwa soko kubwa ambalo Logitech tayari wanalo sasa na pia wataweza kutumia miundombinu ya kampuni hiyo kubwa.
Katika technolojia kununua kampuni ndogo yenye teknolojia ambayo hauna ni moja ya njia za kupata teknolojia ambazo kampuni yako haina, walichofanya Logitech ni kuipata teknolojia ya spika za wireless kwa kuinunua kampuni ambayo inaheshimika katika sekta hiyo.
Hapa kwetu Afrika mashariki mambo haya pia yamekuwa yakifanyika na mfano wake ni pale ambapo kampuni ya Vodacom ilinunua M-paper ambayo ilikuwa kampuni inayofanya vizuri katikamambo ya habari za kidigitali.
Vyanzo: Gadgets 360 pamoja na vyanzo vuingine vya mtandaoni.