Kuroot ni nini? Kuroot simu ya Android ni jambo linalofungua geti kuu la programu endeshaji hiyo na hivyo kukuruhusu kufanya mambo mengi zaidi katika programu endeshaji hiyo kuliko ilivyo kawaida.
Tushaulizwa mara kadhaa juu ya jambo hili na ata baadhi kuuliza jinsi ya kuroot simu zao. Haya ni yote ya kufahamu kuhusu ‘rooting’.
Kwa kiurahisi
Kama wewe ni mtumiaji wa kompyuta ya Windows basi utakuwa unafahamu ya kwamba pale kompyuta ikiwashwa inakupa chaguo la kuingia kama mtumiaji mkuu yaani Administrator – ambapo ukiingia kama Administrator unaweza fanya mengi zaidi katika upakiaji wa programu na ata katika masuala ya mafaili.
Pia kuna uwezo wa kuingia kama Mtumiaji Mgeni – yaani Guest. Ambapo hapa hautaweza fanya mabadiliko mengi katika kompyuta hiyo, utabanwa katika mambo mengi yanayohusu uwekaji programu na ata kufanya mabadiliko ya mipangilio (settings) ya kompyuta hiyo.
Toleo la Android katika simu yako – iwe Samsung, Huawei, Tecno n.k linavyokuja linakuwa linakupa uwezo wa kufanya mabadiliko ya kama mtumiaji mgeni (Guest) katika simu hiyo.
Tendo la kuroot ndilo litakalokupa uwezo wa mtumiaji mkuu, yaani Administrator katika simu hiyo na hivyo utaweza fanya mengi ata yale yanayoweza haribu kabisa programu endeshaji hiyo.
Je utaweza fanya yapi kutokana na kuroot simu yako?
Ukiroot programu endeshaji ya Android ya simu yako utaweza kufanya mambo kama vile
- Kuweka apps ambazo kwa hali ya kawaida isingewezekana kabisa kuwekwa kwenye simu
- Kufuta (delete) apps na programu zilizokuja na simu husika ambazo kwa kawaida huwa huwezi zifuta. Apps hizi zinaitwaga Bloatware
- Kusasisha au kubadilisha kabisa toleo lako la Android. Ata kama mtengenezaji simu husika, iwe Samsung n.k bado hajakupa sasisho rasmi kwa ajili ya simu yako kuweza kupata toleo la kisasa zaidi la Android, kwa kuroot unaweza fanikiwa kupakia toleo la kisasa au ata kubadili kabisa
- Kufanya mabadiliko mengine mbalimbali kulingana na utakacho katika muonekano na utendaji kazi wa simu yako
Njia za Kuroot
Kuna njia nyingi sana kwa sababu suala la kuroot simu linategemea mambo mengi sana, mara nyingi njia ya kuroot simu flani haifanani na ya kuroot simu nyingine. Tofauti zinakuwa kwa kampuni kwa kampuni ya simu na ata saa nyingine tofauti zinakuwa kwa aina ya simu ata kama zinatoka kampuni moja.
Katika kuroot kwenyewe bila kujalisha app au programu au hatua utakazotumia, njia kuu ni mbili;
- Ya kutumia makosa ya programu endeshaji – Kupitia kufahamu makosa, yaani ‘exploits’ basi watengenezaji apps au programu wanaweza fanya programu/app iingie ndani kabisa ya Android ya simu yako na kukupa uwezo wa Admin, yaani simu ikawa ‘rooted’
- Kwa kuweka ‘Custom Recovery’ – Hii ni njia isiyo salama zaidi kwa kifaa chako ila pia ndiyo moja ya njia inayokuwa mara nyingi tofauti tofauti kwa kila kifaa.
Muhimu kufahamu
- Makampuni yenyewe ya simu sio yanayotoa njia za kuroot na kwa kiasi kikubwa huwa hawashauri ufanye jambo hili. Kama simu ina warranty basi kitendo cha kuroot kitaondoa sifa ya warranty hiyo.
- Ukikosea njia au ata kama umefanya kila kitu sahihi kama mambo yasipoenda vizuri basi Android inaweza nasa katika hali inayoifanya simu yako isiweze tumika. Hali hii inaitwa ‘Brick’ – yaani jiwe. Mara nyingi hii inamaanisha itakubidi uanze upya.
Tutakuletea njia mbalimbali maarufu za kuroot simu lakini kama unajiamini na unataka fanya mwenyewe basi mtandao wa XDA ni moja ya sehemu muhimu ya kuanzia. Kitu muhimu sana ni kuhakikisha unafuata maelekezo na kutumia mafaili husika kama maelezo ya jinsi ya kuroot simu hiyo husika. Njia hazifanani.
Je ushawahi kuroot simu yeyote? Waambie wengine ilikuwa ni simu gani na ulitumia njia gani?
Kuhusu kuroot simu mbalimbali na programu zake – Tafuta kwenye mtandao wa XDA – http://forum.xda-developers.com/