Sam Altman apigwa chini. Mkurugenzi Mtendaji wa OpenAI, kampuni ya ubunifu wa akili bandia nyuma ya ChatGPT, ameondolewa kwenye wadhifa wake. Uamuzi huu wa ghafla umechukua tasnia ya teknolojia kwa mshangao, na kuacha maswali mengi yasiyo na majibu ya haraka.
OpenAI ilitoa taarifa ikisema kuwa uamuzi wa kumtoa Altman ulifanywa baada ya “uchunguzi wa kina ambao uligundua kuwa hakuwa mkweli kila wakati katika mawasiliano yake na bodi, na kuzuia uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake.” Bodi hiyo ilisema kwamba haina tena imani katika uwezo wake wa kuendelea kuongoza OpenAI.
Altman alijibu kwenye jukwaa la kijamii la X, akisema kwamba “amefurahia muda wake wote akiwa OpenAI.” akisema walichofanya ana amini kimeleta mabadiliko na maendeleo makubwa kwa yeye, timu nzima na ulimwenguni.
Tetesi: Inasemekana baadhi ya maendeleo ya kibiashara na maboresho ambayo amekuwa akiyasukuma kwenye timu ya utengenezaji yamekuwa hayaendani na hatua za kuhakikisha usalama. Teknolojia ya AI (hasa Generative AI) tayari imeleta hofu kwa baadhi ya watafiti, wakidai ikiendelezwa bila usimamizi mzuri inaweza leta madhara ya kiuchumi, na kiusalama. Open AI inasimamiwa na bodi inayohusisha mashirika yasiyo ya kibiashara yenye lengo la kusimamia usalama wa maendeleo ya teknolojia hiyo.
Altman amekuwa mtu muhimu katika tasnia ya AI, akiwa amesimamia utengenezaji na ukuaji wa teknolojia ya AI kupitia huduma ya ChatGPT, chatbot ya AI ambayo inaweza kuzalisha maudhui ya kiwango cha binadamu kwa kasi ya sekunde. ChatGPT imekuwa ikisifiwa kwa uwezo wake wa kutengeneza kazi za kiubunifu kama vile hadithi, mashairi, na hata sanaa. Pia ni teknolojia inayoweza kutumika katika kurahisisha uharaka wa kazi maofisini na kwenye tafiti.
Uondoaji wa Altman unaweza kuwa na athari kubwa kwa OpenAI. Kampuni hiyo iko katikati ya ukuaji mkubwa, na inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa makubwa ya teknolojia kama vile Google na Microsoft. Altman alikuwa mtu wa kuhamasisha, na alikuwa na uwezo wa kuwavutia watu wenye vipaji vya juu kwenye ajira za kampuni hiyo.
No Comment! Be the first one.