Mabadiliko yanafanyika kwenye huduma namba moja ya kuangalia filamu na tamthilia mtandaoni, Netflix. Kuanzia Oktoba Netflix wataanza kuachia baadhi ya show zake sehemu (episode) moja kwa wiki badala ya kuachilia msimu mzima kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa tamthilia zao nyingi.
Kwa kawaida ilikuwa imezoeleka Netflix kujichukulia sifa ya kuwa sehemu ambayo msimu mzima wa tamthilia unaweza achiwa kwa wakati mmoja – hasa hasa kwa tamthilia zinazotengenezwa na wao (Netflix).

Ila imeonekana wamegundua uamuzi huo hauna manufaa katika kujenga umaarufu wa tamthilia zao ukilinganisha na kama ingekuwa wanaachilia sehemu (episode) moja moja – kila wiki, ukilinganisha na tamthilia kama za Game of Thrones. Inaonekana ile hali ya kusubiria toleo jipya linajenga sana umaarufu wa tamthilia husika kuliko kama zote zitapatikana kwa wakati mmoja.
Pia kimapato inaonekana uamuzi huo si mzuri kwani unafanya baadhi ya watu kuona wanaweza kulipia huduma ya Netflix pale tuu msimu flani unapoachiwa (wa tamthilia wanayoipenda) na hivyo kumaliza kutazama msimu ndani ya siku chache na kuacha kufanya malipo mengine baada ya hapo.
Wengi wanaamini tamthilia (series) ya Game of Thrones iliyokuwa inatengenezwa na HBO kama ingekuwa inaachiwa msimu mzima mara moja jambo hilo lingewaharibia kiasi flani.