Muanzilishi wa kampuni ya Apple watengenezaji wa simu maarufu za iPhones, tableti za iPad na kompyuta za Mac alikuwa ni mtu maarufu na mwenye misimamo mbalimbali ambayo kwa kipindi kingine ilikuwa ni vigumu kumbadilisha. Ila ni kutokana na misimamo yake mbalimbali ndiyo iliyosaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mafanikio mbalimbali kwa kampuni ya Apple.
Katika kipindi kirefu cha uongozi wake wa kampuni ya Apple alifanikiwa kusimamia misimamo yake kwa kiasi kikubwa lakini baada ya yeye kuachia uongozi na baadae kufariki mwaka 2011 uongozi mpya wa kampuni hiyo umejikuta ukifanya mambo mengi ambayo Steve Jobs alisema kamwe kampuni hiyo hayatafanya.
Leo fahamu mambo hayo.
>Simu za umbo kubwa:
Steve Jobs hakuwa anaamini kabisa katika utengenezaji wa simu zenye umbo kubwa/pana. Mwaka 2010 aliikejeli simu za Samsung za Galaxy S akisema ni kubwa sana yaani ata kubebeka mkononi ni shida. Alisema, ‘Hakuna atakayenunua simu hizi’, lakini miezi michache baadae mauzo ya simu za Galaxy S yalikuwa juu sana.
Na kampuni ya Apple iliongeza urefu wa simu zake kupitia toleo la iPhone 5 mwaka mmoja baada ya kifo cha Steve Jobs, na hivi karibuni wakaleta ata iPhone zenye umbo kubwa zaidi kupitia iPhone 6 Plus.
>Tableti za iPad zenye umbo dogo
Mwezi wa 10 mwaka 2010 akiwa katika mahojiano flani Steve Jobs aliponda tableti za Android nyingi zilizokuwa zinaingia sokoni zikiwa katika kipimo cha inchi 7, wakati huo tableti za Apple, yaani iPad zilikuwa ni inchi 10. Alidai ukubwa wa inchi 10 ndio sahihi kabisa kwa ajili ya utumiaji wa apps kwa ufanisi na uzuri zaidi katika tableti, alidai inchi 7 ni ndogo sana na kamwe kampuni ya Apple haitatengeneza tableti chini ya inchi 10.
Mwaka mmoja baada ya kifo chake kampuni ya Apple iliingiza sokoni tableti ya iPad Mini, ambayo ni ya inchi 7. iPad Mini ndiyo tableti inayouzika zaidi kutoka Apple kuliko zinginezo zote.
>Utumiaji wa ubunifu na muonekano wa kihalisia zaidi!
Kama umesikia kitu kinaitwa ‘Flat design’ ambao ni muonekano wa kibunifu unaotumika sana siku hizi kwenye ubunifu wa muonekano wa vitu kama vile apps na n.k katika simu zetu na ata kwenye mitandao ya intaneti fahamu ya kwamba huu ni ubunifu mpya unaojali urahisishaji wa alama za muonekano na kutojali kuonakana sana kama vile kitu kilivyo – yaani uhalisia. Kama utakuwa unakumbuka vizuri zamani kwenye simu ata kwenye mitandao ya intaneti vitu vilikuwa vinaonekana kiuhalisia zaidi, mfano app ya uandishi (Notebook) katika simu na tableti za Apple ilikuwa na muonekano kama wa daftari vile… Steve Jobs alikuwa ni mtu anayeamini katika ubunifu wa aina hii, ubunifu wa muonekano wa kihalisia zaidi, alitaka vitu vionekane kama vile vinavyoonekana katika ulimwengu wa kawaida.
Mwaka mmoja baada ya Steve Jobs kufa kampuni ya Apple ilimfukuza mbunifu mkuu aliyekuwa anafanya kazi kipindi cha Steve Jobs na kumleta mtu mwingine na baadae ndiyo toleo la iOS 7 likaja na muonekano mpya wa ‘Flat Design’. Muonekano huu unajali kuraisisha ubunifu na cha msingi kinakuwa ni kwenye kuleta mvuto zaidi na si kukazania kuleta uhalisia zaidi.
>Apple na utaratibu wa kuchangia na kutoa misaada kwa jamii
Ingawa Steve Jobs alikuwa ni moja ya watu waliopata utajiri mkubwa sana kutokana na uwepo wa kampuni ya Apple, Steve Jobs aliondoa kabisa utaratibu wa kampuni hiyo kutoa misaada kwa jamii mwaka 2007, miezi michache baada ya kupewa uskani tena wa kuendesha kampuni hiyo. Kipindi hicho alidai ya kwamba anafanya hivyo ili kuisaidia kampuni hiyo kuanza kutengeneza faida ila ukweli ni kwamba ata baada ya kampuni hiyo kuanza kutengeneza faida ya mabilioni ya dola za kimarekani bado Steve Jobs hakurudisha utaratibu huo.
Mwaka 2011 miezi michache baada ya Bwana Steve Cooks kuchukua uongozi wa kampuni hiyo baada ya Steve Jobs alirudisha utaratibu huo. Hadi sasa kampuni hiyo ipo kwenye utaratibu mzuri wa kutoa misaada kwa jamii.
>iPad yenye kalamu spesheli – Stylus
Stylus ni mfumo wa peni ya elektroniki inayokuwa inatumika katika kifaa kama vile tableti na ata baadhi ya simu janja. Katika mwaka 2007 wakati Steve Jobs anatambulisha simu mpya ya iPhone katika kipindi hicho alitania sana simu kutoka kampuni zingine zilizokuwa zinakuja na kifaa hicho, alitania akisema watu tayari wana vidole kumi na hivyo hawaitaji cha kumi na moja. Alisema na watu huwa wanapoteza kifaa kama hicho muda si mrefu. Alisema Apple hawatatengeneza kifaa chenye kutumia teknolojia hiyo kamwe!
Na sasa miaka michache baadae tayari inasemekana kampuni ya Apple wapo njiani kutambulisha toleo la iPad Pro, na inasemakana kupitia vyanzo vingi vya uhakika ni kwamba iPad Pro itakuja na teknolojia hii ya Stylus!
Upo hapo? Je ni lipi ulikuwa hulifahamu kabla? Tuambie maoni yako, je unakubaliana na mabadiliko haya?
One Comment